Zitto: Serikali inadumaza kilimo..
Zitto Kabwe, Kiongozi wa ACT Wazalendo
Chama cha ACT Wazalendo kimeiomba serikali kutimiza ahadi yake ya kuwasaidia wananchi wa Kusini pembejeo za kilimo ili kunusuru zao la korosho ambalo kwa kiasi kikubwa linachangia pato la taifa.
Katibu wa itikadi, mawasiliano ya umma na uenezi wa ACT Wazalendo Ado Shaibu amesema serikali kupitia wizara ya kilimo iliwaahidi wananchi wa Kusini kuwapatia pembejeo bure mwezi Mei mwaka huu katika kikao cha mwaka cha wadau wa korosho kilichofanyika mkoani Dodoma lakini ahadi hiyo haijatekelezwa hadi sasa.
Shaibu amesema baada ya serikali kutangaza kugawa pembejeo bure, baadhi ya vyama vya ushirika ambavyo vilikuwa vinanunua na kugawa pembejeo hizo kwa wananchi vimelazimika kurudisha fedha kwa wanachi hao hali ambayo imeleta athari kwa wakulima hao ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa bei ya pembejeo kwa hivi sasa.
Katika mapendekezo yake, chama hicho kimeitaka serikali kununua pembejeo zote na kuzigawa bure kwa wakulima, kuwachukulia hatua wafanyabiashara wanaopandisha bei za pembejeo, kuchunguza ubora wa salfa inayogawiwa ambayo inalalamikiwa na wakulima kwa kuwa na ubora duni pia kimetaika serikali ichukue hatua kali dhidi ya wafanyabiashara wanaochanganya unga wa nafaka kwenye salfa ili kujiongezea faida.
ZITTO NAYE ALONGA
Naye kiongozi wa chama hicho Zitto Kabwe amesema kuwa ili nchi kama Tanzania iendelee inahitaji ukuaji wa kilimo (sekta inayoajiri 65.5% ya watanzania wote) kwa kiwango cha 10% kwa miaka mitatu mfululizo, kisha ukuaji wa 6% kwa miaka mingine 10.
“Tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani ukuaji wa kilimo umedumaa zaidi, kwa mwaka jana kilimo kikikua tu kwa 0.6%, lakini uzalishaji wa korosho ulikuwa kwa zaidi ya 70%, wakulima wa korosho, hasa watu wa kusini, mlilifuta machozi taifa, mkituingizia fedha za kigeni zaidi ya dola milioni 340. Inasikitisha sana kwamba serikali sasa inataka kuwafukarisha, haithamini mchango wenu huu” Amesema Zitto.
Zitto amefafanua kuwa taarifa iliyotolewa leo inahusisha utafiti uliofanywa na viongozi wa chama cha ACT Wazalendo wa ngazi ya majimbo katika mikoa mitano ya Lindi, Mtwara, Pwani, Ruvuma na Tanga kupitia mazungumzo yao na wakulima wa korosho katika mikoa hiyo mitano inayolima korosho zaidi nchini kutafiti hali ya upatikanaji, usambazaji na ugawaji wa pembejeo.
Source:Azamtv
Maoni
Chapisha Maoni