Makanisa mitaani yaliza wakazi Moshi..

Ujenzi wa makanisa katika maeneo ya makazi ya watu kwenye mji wa Moshi mkoani Kilimanjaro umehojiwa na wananchi, huku wakitaka mamlaka zichukue hatua inayostahili kudhibiti utitiri huo.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hii, baadhi ya wakazi wa Moshi wamesema ingawa zipo mamlaka zinazohusika, lakini zimefumbia suala muda mrefu na hivyo kuibua sintofahamu kubwa.
John Bennett amedai kuwa baadhi ya makanisa katika eneo hilo yanaanza shughuli pasipo kufuata mchakato wa kisheria wa kubadilisha matumizi ya ardhi kwanza.
“Kuna kanisa hapa limeanza mwaka 2003 bila kubadili matumizi ya ardhi kwanza kama sheria ya mipango miji inavyosema hadi mwaka 2013 ndio wakaomba kubadili matumizi ya ardhi,” amedai.
“Kuna nyumba zikianza tu kama hujafuata kibali unaletewa stop order (zuio) lakini makanisa haya yameanzishwa maeneo ambayo hayakupangwa kwa ajili hiyo na Halmashauri wapo,”amelalamika mkazi huyo.
Kwa mujibu wa Bennett, wakati wakiendelea kupinga kanisa hilo kumeibuka kanisa lingine linaloendesha shughuli zake katika maeneo hayo katika ofisi za chama kimoja cha siasa.
“Sisi kama majirani hatujawahi kushirikishwa kuwa maeneo hayo sasa yanakuwa makanisa. Yameweka vipaza sauti ni kelele mchana na usiku. Uhuru wa kuabudu usiwe kero kwa wengine,” amelalamika.
Mkazi mwingine wa mjini Moshi, James Karua anayemiliki vituo vya mafuta, amesema katika eneo analoishi kuna kanisa limeanzishwa na kusababisha usumbufu mkubwa kwa majirani wanaoishi jirani na kanisa hilo.
Meya wa Manispaa ya Moshi, Raymond Mboya ameonya wimbi la uanzishwaji holela wa makanisakatikati ya makazi ya watu akisema ni kinyume cha taratibu.
“Hata vitabu vya dini vinaelekeza kuheshimu mamlaka. Tuna sheria ni lazima waombe kubadili matumizi ya ardhi husika na siyo kuanzisha popote wanapojisikia,” amesema Mboya.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Januari Makamba ameahidi kutuma wataalamu wa mazingira mjini Moshi, kuchunguza malalamiko ya wananchi hao huku akisema sheria za uchafuzi wa mazingira ziko wazi kuwa ni pamoja na viwango vya sauti vinavyoruhusiwa na visivyoruhusiwa katika maeneo ya makazi.


Source:Mwananchi

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

USAJILI WENYE MANUFAA EPL HADI SASA..