PROF. LIPUMBA KUENDELEA KUNG’OA WABUNGE WA MAALIM, AMUONYA KUBENEA..
Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, amesema Kamati ya Maadili na Nidhamu inayomuunga mkono inaendelea na ngwe ya pili ya kuhoji wabunge wa majimbo wanaomuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Shariff Hamad, kwa madai ya kuwa na utovu wa nidhamu.
Prof. Lipumba ameyasema hayo leo Julai 27,2017 wakati akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kupata taarifa kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa CUF, za kuhudhuria mkutano wa baraza hilo kesho mjini Zanzibar, zilizotolewa na Joran Bashange aliyejitambulisha kama Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho.
Aidha, amelishukuru Bunge kwa kuridhia maamuzi ya Baraza la Uongozi linalomuunga mkono ya kuwavua uanachama wabunge nane wa viti maalumu, ambapo amesema majina ya watakaorithi nafasi hizo yameshapelekwa bungeni.
Katika hatua nyingine, amemshukia Makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Saed Kubenea kutokana na Operesheni aliyoanzisha ya ‘Ondoa Msaliti Buguruni’ iliyolenga kumng’oa madarakani, na kueleza kwamba ana uwezo wa kumshughulikia kiongozi huyo, lakini anafuata taratibu za kisheria.
“Kubenea ningeweza kumshughulikia mara moja, lakini nafuata utaratibu wa kisheria, ningeamua kuwaita ulingoni yeye na Sumaye wake halafu Maalim akawa refa tukapambana ningewashinda,” amesema.
Licha ya hayo, Lipumba ametoa wito kwa vyombo vya dola kuwachukulia hatua baadhi ya viongozi wa chama hicho anaodai ametengua nyadhifa zao, wanaoendelea kufanya shughuli za CUF.
Amedai kuwa, Bashange pamoja na baadhi ya viongozi wengine aliotengua nyadhifa zao wanaoendelea kufanya shughuli za chama hicho, wanakiuka sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 kifungu cha 8B (2) kinachokataza mtu asiye kiongozi wa chama cha siasa kufanya shughuli ya chama husika kama kiongozi wake.
Kuhusu Katibu Mkuu CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, amedai kuwa kwa sasa hatakiwi kufanya shughuli za chama hicho hadi atakapo kubali kufuata maelekezo yake kutokana na Katibu huyo kushindwa kutekeleza majukumu yake. Na kwamba Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Katibu Mkuu ni Magdalena Sakaya, kama katiba ya chama hicho inavyoelekeza endapo Katibu Mkuu ameshindwa kutekeleza majukumu yake.
“Kwa makusudi Bashange anavunja sheria ya vyama vya siasa, anafanya kosa la jinai akipelekwa mahakamani faini ni milioni moja au kifungo cha miezi sita jela, vyombo vya dola vinapaswa kumchukulia hatua kwa kukiuka sheria ya vyama vya siasa…Katiba yetu inatambua kuwa Katibu Mkuu siyo mtu bali ni ofisi, Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Katibu Mkuu hivi sasa ni Magdalena Sakaya ambaye ni Kaimu Katibu Mkuu,” amesema.
Hata hivyo, amesema maamuzi yatakayotolewa na kikao cha baraza hilo hapo kesho ni batili kwa madai kuwa yeye ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Taifa, hajakiitisha na wala kupewa taarifa za kuitishwa kwa kikao hicho.
“Maalim Seif ndiyo aliyewaponza wabunge waliovuliwa ubunge, mliobakia msiwe mnafuata anachokisema Katibu Mkuu,” amesema.
Source:Modewjiblog
Maoni
Chapisha Maoni