Waziri Mkuu azindua Wakala wa Barabara Vijijini
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiashiria uzinduzi wa TARURA
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) na kusema changamoto ya usafiri nchini, hususan maeneo ya vijijini inatarajiwa kuwa historia.
Waziri Mkuu amefanya uzinduzi huo leo katika ukumbi wa Chuo cha Mipango, mjini Dodoma na kusema wakala huo utasaidia kuimarisha mtandao wa barabara za vijijini na kuwawezesha wananchi wengi kusafiri na kusafirisha bidhaa zao kwa urahisi na kukuza uchumi.
"Wakala huu tunaouzindua leo utakuwa na manufaa makubwa kwa ustawi wa nchi yetu kwa kuongeza chachu ya uzalishaji mali mashambani kutokana na urahisi wa kufika sokoni, utashusha bei ya vyakula mijini na bidhaa za viwandani vijijini kutokana na gharama za usafirishaji wa mazao kutoka mashambani na bidhaa za viwandani kutoka mijini kupungua," alisema Waziri Mkuu
Awali, Waziri wa TAMISEMI, George Simbachawene alisema TARURA ni muhimu kwa kuwa inagusa wananchi moja kwa moja na ni kichocheo kikubwa cha uchumi wa wananchi, hivyo kuinua uchumi wa taifa wenye msingi imara.
Kutokana na umuhimu wa mtandao wa barabara za Vijijini na Mijini, Simbachawene ameomba mgawanyo wa mapato ya Mfuko wa Barabara wa asilimia 70 kwa TANROADS na asilimia 30 kwa Halmashauri uangaliwe upya, ambapo Waziri Mkuu ameridhia.
Mtandao wa barabara za Mamlaka ya Serikali za Mitaa ni kilomita 108,942.2 ambao ni Zaidi ya nusu ya barabara za Kitaifa.
Source:AzamTv
Maoni
Chapisha Maoni