Balozi Seif atembelea uwanja wa Mao Tse Tung.
Mhandisi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Ali Mbarouk (katikati) akimuonyesha Balozi Seif, ramani ya uwanja wa Mao Tse Tung utakavyokuwa baada ya kukamilika.
MATAYARISHO ya ujenzi wa kiwanja cha michezo cha Mao Tse Tung, Mjini Zanzibar, yameanza rasmi kwa hatua ya utafiti wa udongo wa eneo hilo.
Mhandisi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Ali Mbarouk alieleza hayo wakati akitoa ufafanuzi kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi aliyefanya ziara fupi ya kukagua matayarisho hayo.
Mhandisi huyo alimueleza Balozi Seif kwamba, utafiti huo wa udongo unafanywa kwa kuchukuwa aina tofauti za udongo kwenye vishimo 34 kwenye eneo la uwanja. Utafiti huo unatarajiwa kuchukuwa muda wa siku 20.
Alisema udongo huo utafanyiwa utafiti wa kina na wataalamu waliobobea na baadaye watatoa ripoti kamili itakayofuatiwa na utangazaji wa tenda kwa makampuni yatayokuwa tayari kujenga uwanja huo.
Alifahamisha kazi ya ujenzi ya uwanja huo inatarajiwa kuanza rasmi mwezi wa Februari mwaka ujao 2016 chini ya ufadhili wa Serikali ya China.
Akitoa ufafanuzi wa ramani ya ujenzi Mhandisi Ali Mbarouk alimueleza Balozi Seif kwamba, uwanja huo utakapomalizika utakuwa na viwanja viwili vya mchezo:
Ali Mbarouk alisema: “Kutakuwa na uwanja wa mpira wa miguu (Football) na kutakuwa na viwanja kwa ajili ya michezo ya mpira wa pete (Netball) na mpira wa kikapu (Basketball).
Aidha, alisema kwamba lipo eneo maalumu kwa michezo mbalimbali ya ndani (INDO GAMES), majukwaa ya watazamaji, jukwaa la watu maarufu (VIP), na ofisi za wafanyakazi.
Akielezea furaha yake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, alisema kukamilika kwa uwanja wa huo kutasaidia kuupunguzia mzigo mkubwa katika uwanja wa Amani.
Balozi Seif alisema uwanja wa Amani kwa sasa ndiyo pekee unaotumika kwa michezo yote ya kimataifa na kitaifa, ikiwemo ya sherehe za Mapinduzi.
Source(Zanzibar Kwanza)
Maoni
Chapisha Maoni