Pinda aunga foleni ya wasaka urais.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akionesha mkoba wenye fomu ya kuwania kuteuliwa na CCM kugombea nafasi ya Urais katika uchaguzi mkuu mwaka huu baada ya kuchukua fomu hiyo, Dodoma jana. Kulia ni mkewe, Tunu Pinda na Katibu wa Oganaizesheni wa NEC, Mohamed Seif Khatib. (Picha na Ofisi Waziri Mkuu)
WAZIRI Mkuu jana amejitosa rasmi kuchukua fomu na kuingia katika kinyang’anyiro cha kuomba kupeperusha bendera ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Pinda, ambaye amekuwa mgombea wa 32 kuomba fursa hiyo ndani ya CCM amesema Mungu pekee ndiye anayemjua mwanachama atakayeteuliwa kugombea nafasi hiyo, huku akitamani Mungu ampe kibali cha kuongoza Watanzania kwani ana lengo la kuwafikia wanyonge.
Pinda alifika Makao Makuu ya CCM saa nne asubuhi akiwa ameambatana na mkewe, Tunu Pinda, huku baadhi ya wabunge wakimsindikiza katika kumuunga mkono kwenye hatua yake ya kuwania nafasi hiyo.
Akizungumza mara baada ya kuchukuwa fomu, Pinda alisema endapo atapata nafasi ya kushika nafasi hiyo ya juu nchini, atazingatia suala zima la mazingira na kuimarisha utawala bora, kwa kuwa hayo ndio nyongeza ya maadui watatu wa asili; ujinga, maradhi na umasikini.
“Ilani yetu haijatoka, humu ndipo kutakuwepo sera, maelezo na mikakati yote, kwa hiyo sina cha kusema mpaka Ilani itakapopitishwa na ikitokea nikateuliwa sitashindwa kuitekeleza na nalisema hili kwa uhakika.
Ufunuo wa Mungu “Kila aliyechukua fomu anataka ateuliwe yeye lakini Mungu pekee ndiye anayemjua, mimi simjui, na wala wenzangu hawamjui, na kila mmoja anasema moyoni mwake kwamba atakuwa yeye na Mungu angemnong’oneza basi angetamba mpaka asubuhi,” alisema.
Alisema katika kuimarisha utawala bora, atajikita katika kuimarisha Taasisi ya Kupambana na Kuzia Rushwa (Takukuru), ikiwa ni pamoja na kuwapa uhuru kamili katika kupambana na watendaji wasio waadilifu, wezi na wala rushwa.
“Watanzania wote tunawajibika kuhakikisha nchi inaongozwa kwa uwazi na kuwa na viongozi wenye maadili ambao wana uchungu na umasikini wa Watanzania.
“Tutaangalia jinsi ya kuipa meno Takukuru, wewe kama sio mla rushwa hauna haja ya kuogopa hili, mtu akipatwa apelekwe mahakamani hakuna hata haja ya kuomba kibali kwa Waziri Mkuu,” alisema.
Rekodi yake
Pinda ambaye ana kaulimbiu ya ‘Uchungu wa mwana aujuae mzazi’ alisema amefanya kazi na marais wa awamu zote, amejifunza mengi na kwamba amekuwa Waziri Mkuu kwa kipindi cha miaka minane akiwa ndiye msimamizi mkuu wa utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Amesema Rais Jakaya Kikwete amefanya mambo mengi, ikiwemo kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo inayoishia mwaka 2025, ambayo iliasisiwa na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa kwa kutekeleza mpango wa miaka mitano wa maendeleo, uliolenga kuboresha miundombinu, ili kila mji na mikoa iunganishwe kwa lami.
Pinda alisema katika uongozi wake, atahakikisha anatekeleza Mpango wa Maendeleo Awamu ya Pili, ambao umelenga kujenga viwanda hususani vya kuthaminisha mazao ya wakulima, wafugaji na wavuvi.
“Kwa kufanya hivyo, tunaweza kunufaisha watu wengi ambao hawajafikiwa na pia itakuwa njia ya kupunguza umasikini kwa wananchi waliowengi na kufikia uchumi wa kati,” alisema.
Alisema uchumi wa Watanzania unakua, lakini bado Watanzania ni masikini kwa kuwa uchumi huo unakua kwa kutegemea sekta ya ujenzi, maliasili na uchukuzi ambazo hazigusi watu wengi.
Ana kipya?
Akijibu swali kuhusu kitu gani kipya anachotarajia kuonesha, wakati amekuwepo serikalini kwa muda mrefu lakini bado kumekuwa na ubadhirifu hasa katika halmashauri, Pinda alisema amefanya mengi lakini hana desturi ya kujisifia.
“Mimi nipo Serikali za Mitaa tangu nilipoingia kwenye siasa, CAG mwenyewe (Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali) anatusifu katika kaguzi zake tofauti na miaka ya nyuma ambapo hali ilikuwa mbaya.
“Hadi sasa tumeshafukuza wakurugenzi watendaji zaidi ya 2,000 bahati mbaya tu mie sina tabia ya kujisifu. “Na kama unadhani huyo ambaye hakuwemo madarakani ndio atakuja na kitu kipya umefanya kosa, kwa kuwa akija ataanza kwanza kujifunza, aelewe na mwisho ataboronga tu.
Akina Magufuli
“Simba mwenda pole ndiye mla nyama nono, tazama hata mawaziri wangu wanavyofanya mazuri, alikuja Muhongo akaondoka (Profesa Sospeter Muhongo, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini). “Mtazame Magufuli (Dk John Magufuli, Waziri wa Ujenzi), mkiwaona hawa jueni kiranja wao ni mimi,” alisema.
Aliwataka Watanzania kutofanya uamuzi usio sahihi kuhusu yeye halafu baadaye wakayajutia. Pinda aliongeza: “Nimeyasimamia yote haya lakini bahati mbaya tu majigambo sina la sivyo ningekuwa mtu wa makeke mbona mngenikoma!” Kuhusu kauli yake aliyowahi kunukuliwa kwamba hautaki urais na kwamba amejiandaa kustaafu kwenda kufuga nyuki, Pinda alisema ni kweli wakati alipotoa kauli hiyo mwaka 2012 hakuwa na ndoto ya urais.
Alisema wakati ule aliwaambia wapigakura wake kwamba miaka 15 ya kuwa mbunge wao inatosha na kwamba hatagombea tena nafasi hiyo. “Lakini hata kama ningekuwa nimesema hivyo hakuna ubaya, wakati ule ilikuwa mwaka 2012 hivyo nikibadili msimamo wangu kuna tatizo gani, hata mke ukimuacha unaweza ukamrudia,“ alisema.
Mimi ni mwanadamu ninaweza nikapata msukumo mwingine, nikashawishiwa na ndugu, marafiki na hata Mwenyezi Mungu, lakini hata hivyo siku zote huwa nasema urais ni jambo kubwa na mimi nimeamua kujitosa katika hili lakini hataka kama nikipata iwe ni kwama mapenzi yake,” alisema.
Waliomsindikiza
Baadhi ya watu walimsindikiza Pinda kuchukua fomu ni pamoja na Mwanasiasaa Mkongwe aliyekuwepo katika Baraza la Mawaziri la Mwalimu Julius Nyerere, Mzee Job Lusinde na aliyewahi kuwa Waziri katika Serikali yaawamu ya tatu, Paul Mzindakaya na Didas Masaburi Meya wa Jiji la Dar es Salaam.
Baadhi ya wabunge waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata, Mbunge wa Igunga, Dk Peter Kafumu, Mbunge wa Viti Maalumu, Dk Pudensiana Kikwembe, Mbunge wa Mtwara Mjini, Hasnain Murji.
Mgombea wa 33
Leo kada wa 33 wa CCM, Dk Mzamini Kalokola kutoka Tanga, anatarajiwa kuchukua fomu ambaye naye alisema: “Nimekuja kwa ajili ya kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya urais kupitia Chama Cha Mapindunzi kwa mwaka 2015,” amesema Dk Kalokola.
Wengine
Makada wengine waliokwisha kuchukua fomu ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, Naibu Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, mkazi wa Musoma mkoani Mara, Boniface Ndengo, mkulima kutoka Kijiji cha Mjimtala Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, Eldefonce Bilohe na Dk Hassy Kitine.
Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Dk Mwele Malecela, Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kingwangala, Balozi, Amina Salum Ally, Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Waziri wa Kilimo na Chakula, Steven Wassira, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal na Waziri wa Ujenzi, John Magufuli.
Wengine ni Balozi Ally Karume, Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya, Mtumishi wa CCM Idara ya Siasa na Uhusiano wa Tanzania Amos Siyantemi, Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, Wakili mwandamizi Mahakama Kuu Tanzania Godwin Mwapango, Peter Nyalile, Leonce Mulenda, Wengine Sospeter Muhongo, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani, Makongoro Nyerere, mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Amos Robert, Balozi Agustino Mahiga na Monica Mbega na Dk Hassy Kitine.
Source()Habari Leo)
Maoni
Chapisha Maoni