Baraza la famasia lakiri kutokusajili kozi ya famasia inayotolewa na chuo cha KIU.
Baraza la famasia nchini limesema halijasajili kozi ya famasia inayotolewa na chuo kikuu cha Kampala kampasi ya Dar es Salaam kwa sababu hakijakidhi matakwa ya kusajiliwa huku uongozi wa chuo hicho ukizungumzia suala hilo.
Msajili wa baraza hilo Bi Zainabu Kamingoma ameyasema hayo katika mahojiano maalum na ITV ambapo amedai kuwa uongozi wa chuo hicho ulikosea tangu awali baada ya kujenga majengo na kuanza kusajili wanafunzi bila ya kushirikisha baraza wala kuomba usajili na kwamba majengo na vifaa siyo kigezo cha wao kupata usajili.
Kufuatia maelezo hayo ITV imeutafuta uongozi wa chuo cha Kampala ili kuzungumzia sakata hilo ambapo naibu mkurugenzi wa udahili wa chuo hicho Bw Lotha Samora mbali na kueleza kushangazwa na kauli ya msajili ameonyesha nyaraka mbalimbali walizopewa na baraza hilo zikiwaruhusu kuendelea kutoa taaluma hiyo na kuhusu wahitimu ambao vyeti vyao havitambuliki wamekubaliana na serikali wavipeleke TCU vikashughulikiwe.
Kwa upande wa wanafunzi walioathiriwa na tatizo hilo ambalo limepelekea mgomo na chuo kufungwa wamesema hawako tayari kurudi darasani hadi watakapopata barua rasmi ya kozi hiyo kutambuliwa kwani lengo la wao kusoma ni ili watambuliwe lakini pia waweze kuingia kwenye soko la ajira.
Hivi karibuni mgogoro huo ulisababisha wanafunzi wa kitivo cha afya chuoni hapo kugoma hali iliyopelekea askari wa kikosi cha kutuliza ghasia kutumia mabomu ya machozia na maji ya kuwasha kuwatawanya na baadhi ya wanafunzi kujeruhiwa katika purukushani hizo.
Source (ITV)
Maoni
Chapisha Maoni