Watu 141 wakamatwa katika msako.

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP, Ernest Mangu.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Ernest Mangu

JESHI la Polisi nchini kupitia Kitengo cha Interpol limewakamata watu 141 kwa makosa mbalimbali kupitia operesheni maalumu iliyofanyika kwa siku mbili kuanzia Juni 4 hadi 5, mwaka huu ikiwa imefanyika kwa wakati mmoja katika nchi 25 wanachama barani Afrika.
Akitoa taarifa hiyo mbele ya waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, CP Diwani Athumani alisema wamekamata jumla ya watuhumiwa 141 katika operesheni iliyopewa jina la operesheni II inayohusisha makosa mbalimbali.
“Taarifa hii inatokana na operesheni tuliyoifanya kwa makubaliano ya Kanda za Polisi ya Interpol kuwa iwepo kwa nchi 25 kutoka Kanda ya Kusini mwa Afrika (Sarpocco) na Kanda ya Afrika Mashariki (EAPCCO) na pia imefanyika kwa siku mbili katika tarehe hiyo kwa nchi zote wanachama,” alisema Athumani.
Alisema walifikia makubaliano hayo ya kuwa na operesheni maalumu itakayofanyika kwa wakati mmoja ili kuweza kukabiliana na matukio mbalimbali ya kihalifu yanayotokea kwa nchi wanachama.
Aidha alisema makosa yaliyopewa kipaumbele zaidi katika operesheni hiyo ni pamoja na wizi wa magari, dawa za kulevya, silaha haramu na milipuko, wahamiaji haramu na biashara haramu ya binadamu, ugaidi, biashara ya madini, wizi wa miundombinu ya umeme na nyara za serikali.
Katika operesheni hiyo waliweza kukagua magari 1,400 na kati ya hayo magari 6 yaliripotiwa kuibiwa na mengine 5 yalionesha kuingiliwa kwenye chesisi pamoja na pikipiki 12 ziligundulika kuibiwa.
Alibainisha kuwa magari yaliyoibiwa yalionesha kutokea nchi mbalimbali ikwemo moja kutoka Afrika Kusini, matatu kutoka England, moja kutoka Hungary, na moja ni kutoka Tanzania.
Katika kitengo cha madawa ya kulevya, walifanikiwa kuteketeza ekari 49 za bangi, kukamata heroini kete 12, kilo 1505 za bangi, na mirungi kilo 68.
Pia walikamata silaha tatu zikijumuisha SMG 1 pamoja na gobori 3 na kufanikiwa kukamata wahamiaji haramu 35 kutoka nchi tofauti.
Wahamiaji haramu waliokamatwa walibainika kutoka mbalimbali ikiwemo mmoja kutoka Ugiriki aliyekamatiwa Zanzibar, 30 kutoka Burundi walikamatwa mkoani Kigoma, mmoja kutoka Nigeria aliyekamtwa mkoani Arusha.
Wengine wawili kutoka Rwanda walikamatwa mkoani Kagera na mmoja kutoka Zambia pia alikamatwa katika Mkoa wa Ruvuma.
Aidha jeshi hilo pia lilikamata vijana wanne wakiwa na CD 8 zenye mafunzo yenye uelekeo wa kigaidi pamoja na madini aina ya ‘Green Quartz’ yenye uzito wa kilo 96 na thamani ya Sh. milioni 7 kutokana na mmiliki wake kutokuwa na kibali.
Source(Habari Leo).














Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

USAJILI WENYE MANUFAA EPL HADI SASA..