Mabomu yatumika kuwadhibiti wanafunzi KIU.
POLISI na askari wa Kikosi Maalumu cha Kuzuia Fujo (FFU) wamelazimika kutumia mabomu ya machozi kutawanya wanafunzi wa Chuo cha Kimataifa cha Kampala (KIU) baada ya wanafunzi wa Fani ya Afya kugoma kuondoka chuoni hapo wakifanya mkusanyiko kulalamikia kuwa fani wanayosoma haijasajiliwa.
Askari hao walifika na kuwatawanya wanafunzi kwa mabomu ya machozi na maji ya kuwasha jambo lililosababisha vurugu na kupelekea baadhi ya wanafunzi kuumia pamoja na baadhi ya wananchi waliokuwa maeneo ya jirani na chuo.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti baadhi ya wanafunzi ambao waliogopa kutajwa majina yao kwa hofu ya kufukuzwa chuo walidai kusikitishwa na uongozi wa chuo hicho kwa kufanyiwa vurugu wakati wanachodai ni haki yao.
“Tunaiomba Serikali isimamie jambo hili kwa kweli tunanyanyasika sana wakati tumelipa ada kubwa na bado fani tunayosoma haijasajiliwa hii si haki kabisa na inatia uchungu,” alisema mmoja wa wanafunzi.
Alisema wanafunzi wanalalamikia usajili wa Fani ya Afya kwa upande wa Maabara na Famasi, kuwe na mtaala unaotambuliwa na TCU, kiwango cha ada wanayolipa ni kubwa na pia malipo ya mitihani inayotakiwa kurudiwa na pia waalimu wengi si Watanzania bali Waganda.
Akielezea tukio la jana alisema wanafunzi wa fani hiyo walifika hapo kwa ajili ya kufanya mitihani yao ambayo ilikuwa ianze jana hata hivyo kuna wenzao ambao waliwapa taarifa kuwa kuna Kamati ya Bunge ambayo itawatembelea kujua matatizo yao hivyo wakaamua kukaa wakiimba wakisubiri kuonana na wabunge.
“Tukiwa tumekaa tunaendelea kuimba alikuja kijana mmoja ambaye ni wa hapo chuoni lakini si mwanafunzi alituambia tuondoke akaanza kutupiga mawe, wanafunzi walikasirika sana lakini baada ya muda walikuja askari na kutuambia tuondoke chuo kimefungwa,” alisema mwanafunzi huyo.
Mwanafunzi mwingine alisema kuwa baadaye waliitwa FFU na kuleta gari la maji na kuanza kuwasambaza wanafunzi ambao walikuwa wamekusanyika kitendo kilichowafanya wasambae na kukimbizana huku na huko huku wengine wakiumia.
Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano wa Chuo cha KIU, Keneth Liki alikiri kutokea kwa vurugu hizo ambapo alisema uongozi wa chuo haupendi kuona hali hiyo ikitokea na kwamba mara kadhaa wamewaelewesha wanafunzi kuwa taratibu zinaendelea za kusajili fani hiyo ya afya zinazolalamikiwa lakini wanafunzi hawataki kuelewa wanaendeleza migogoro.
Source(Habari Leo)
Maoni
Chapisha Maoni