Afisa wa Wizara ya Afya akutwa amefariki kwenye nyumba ya kulala Wageni Pemba....

AFISA uhamasishaji kutoka Wizara ya Afya kitengo cha Malaria Zanzibar Mohammed Yussuf Mkanga (54) amekutwa  akiwa amefariki dunia  katika nyumba ya kulala wageni  Bomani inayomilikiwa na Shirika la Bandari Zanzibar tawi la  Pemba .

Taarifa ambazo zimepatikana na mwandishi wa habari hizi zinasema kuwa Mkanga akiwa na watendaji wenzake wa kitengo cha malaria  waliwasili katika nyumba hiyo siku ya Jumatatu ya tarehe 21 septemba 2015 majira ya saa kumi na moja za jioni .

Akizungumza katika eneo la tukio , Msaidizi  Meneja kitengo cha Malaria Zanzibar Mwinyi Issa Msellem amesema kuwa tangu walipowasili katika nyumba hiyo  hali ya Mkanga ilikuwa nzuri na hakukuwa na taarifa zozote za kusumbuliwa na maradhi .

Mwinyi ameeleza kwamba kikawaida Mohammed Yussuf Mkanga  alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya Sukari na Presha lakini mwenyewe alikuwa amepata taaluma ya kudhibiti maradhi hayo .

"Mkanga tangu tunafika Pemba hali yake ilikuwa nzuri na hakukuwa na taarifa ya kusumbuliwa na maradhi yoyote , kiuhalisia  alikuwa na maradhi ya sukari na Presha lakini mwenyewe alikuwa na uwezo wa kuyadhibiti maradhi hayo " alifahamisha Mwinyi .

Naye Khamis Ameir Haji afisa wa Afya kutoka Kitengo cha malaria Zanzibar ambaye alikuwa amefuatana na Marehemu amefahamisha kwamba wamekuja Kisiwani Pemba kwa ajili ya mkutano wa kuwashukuru wadau waliofanikisha kampeni ya upigaji wa dawa majumbani .

Ameeleza kwamba  katika mkutano huo ambao ulikuwa uwashirikishe wadau mbali mbali wakiwemo wandishi wa habari pia ulikuwa na lengo la kuliaga Shirika la RTI International ambalo limekuwa likisaidia kampeni hiyo ya upigaji wa dawa majumbani .

"Tulikuja Pemba kwa ajili ya kuwashuruku wadau waliotuunga mkono katika kampeni za upigaji wa dawa majumbani pamoja na kuliaanga Shirika la RTI International la Marekani ambalo lilifadhili kampeni hiyo " alieleza Khamis Ameir Haji.

Mlinzi wa nyumba hiyo Salim Khamis Salim (59) Mkaazi wa Gando Mabatini amesema kuwa marehemu Mkanga aliingia ndani ya chumba chake majira ya saa tatu usiku na kuanzia muda huo hakuwahi kutoka nje .

Alifahamisha kwamba akiwa pamoja na Wageni waliokuwa wamelala katika nyumba hiyo waliipata wasiwasi baada ya kufika saa mbili asubuhi na walipochungulia walimuona akiwa amelala , ambapo juhudi za kugonga mlango ili afungue hazikuzaa matunda .

"Aliingia ndani ya chumba alichokuwa amelala majira ya saa tatu usiku na kuanzia muda ule hakutoka nje na tulipata mashaka ilipofika saa mbili za asubuhi baada ya wenzake kuamka na kumaliza kunywa chai , tuligonga mlango bila mafanikio "alifahamisha .

Tukio hilo limethibitishwa pia na kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Shekhan Mohammed Shekhan ambaye ameeleza baada ya kupata taarifa walilazimika kuvunja mlango na kumkuta akiwa amefariki dunia .

Mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi na daktari dhamana Hospitali ya Wete Othman Maalim Haji kasha kusafirishwa kwenda nyumbani kwake Chwaka kwa ajili ya mazishi .




SOURCE:ZanziNews






















Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

USAJILI WENYE MANUFAA EPL HADI SASA..