KASHFA YA JINAI FIFA:Blatter aanza kuchunguzwa...


Hatimaye maofisa upelelezi wa polisi wameanzisha uchunguzi juu ya kuhusika kwa Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Sepp Blatter kwenye makosa ya jinai yanayohusisha rushwa, wizi na utakatishaji wa fedha.
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu (AG) wa Uswisi imeeleza kwamba sasa bosi huyo aliyekubali kuachia ngazi baadaye, amefunguliwa rasmi jalada la jinai na uchunguzi unafanyika, akituhumiwa kuhusika na vitendo vya jinai kwenye uongozi wake, ikiwamo wizi wa fedha.
Uchunguzi huo umefika mbali kiasi cha kumhoji Blatter mwenyewe, lakini pia maofisa wa polisi kuingia na kupekua ofisi yake, na taarifa ya Fifa imesema kwamba wanatoa ushirikiano wote unaotakiwa kwa ofisi hiyo ya AG.
Wapelelezi wanasema kwamba uchunguzi unalenga mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na yanayozunguka dili za  haki za televisheni, ambazo Blatter amesaini sambamba na aliyekuwa Mkuu wa Shirikisho la Soka la Caribbean, Jack Warner mwaka 2005.
Warner yupo kwenye kundi la watu 14 ambao Mei mwaka huu walifunguliwa majalada na makachero wa Marekani na sasa mchakato uliokuwa ukiendelea ni wa kuwahamishia watuhumiwa wote Marekani kwa ajili ya kujibu kesi zao.
Taarifa ya AG inasema kwamba Blatter anatuhumiwa kutoa malipo yasiyo sahihi mwaka 2011 kwa Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa) chini ya Rais Michel Platini. Maofisa saba wa Fifa walikamatwa jijini Zurich kabla ya mkutano wa Mei 29 uliomchagua tena Blatter kuwa rais lakini siku nne baadaye akasema angeachia ngazi kwa sababu anaona haungwi mkono na ulimwengu wote wa soka.
Blatter amekuwa akitarajiwa kwamba ataachia kiti chake Februari mwaka kesho, kwani ameagiza kuitishwa kwa mkutano maalumu wakati yeye akiendelea na kile anachokiita kukamilisha mchakato wa mageuzi makubwa ndani ya shirikisho hilo. Amepata kushauriwa kuondoka madarakani mara moja, lakini akakataa.







SOURCE:Tanzania Sports













Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

USAJILI WENYE MANUFAA EPL HADI SASA..