Sikukuu ya eid el hajj kufanyika kitaifa Mkokotoni Wilaya ya Kaskazini Unguja..
Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar Abubakar Khamis Bakar akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani) Ofisini kwake Mazizinni, kuhusu Sherehe ya Sikukuu ya Idd el Hajj zitakazofanyika siku ya Alkhamis tarehe 24.9.2015 katika Kijiji cha Mkokotoni Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja.
Waandishi wa Habari wa vyombo mbali mbali wakimsikiliza Waziri wa Katiba na Sheria Aboubakar Khamis Bakar alipokuwa akitoa taarifa ya Sikukuu ya Idd el Hajj itakayofanyika Mkokotoni Wilaya ya Kaskazini Unguja.
WAZIRI wa Katiba na Sheria Zanzibar Aboubakar Khamis Bakar amewataka wakaazi wa shehia za Wilaya ya Kaskazini ‘A’ kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya sherehe za Idd el Hajj zitakazofanyika Kitaifa Mkokokotoni. Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Akizungumza na waandishi wa Habari Ofisini kwake Mazizini, Waziri Aboubakar amesema kufanyika kwa sherehe za Idd el Hajj ndani ya Wilaya za Unguja na Pemba ni kutokana na uwamuzi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mpinduzi Dkt. Ali Muhamed Shein ili wananchi wote wa Wilaya na Mikoa kupata fursa ya kukutana na viongozi wao wakuu wa kitaifa.
Alisema sala ya Idd el Hajj itasaliwa katika kiwanja cha Mpira cha Mkokotoni Polisi na Baraza la Idd litafanyika Ukumbi wa Chuo cha Amali.
Waziri Aboubakar alisema katika kusherehekea sikukuu hiyo Serikali bado inasisitiza kuendeleza tabia njema ya kulinda heshma katika jamii ya kizanzibari wakati wote ikiwemo kuvaa nguo za heshma na watoto kusherehekea sikukuu wakati wa mchana.
Aliagiza disko toto ni marufuku na muda wa mwisho wa sherehe katika viwanja vyote vya sikukuu Unguja na Pemba itakuwa ni saa 4.00 usiku
Aidha Waziri wa Katiba na Sheria amepiga marufuku aina yoyote ya disko kupigwa katika viwanja vya wazi pahala popote na disko zinazoruhusiwa ni zile zitakazopigwa katika kumbi zilizoruhusiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa na Baraza la sanaa,
Aliwaomba wazazi kuacha tabia ya kuwaruhusu watoto wadogo kwenda katika viwanja vya sherehe wakiwa peke yao ama kuwafuatanisha na watoto wenzao kwani kufanya hivyo kunaweza kutoa nafasi ya kutokea uhalifu na udhalilishaji wa watoto hao.
Mwaka jana maadhimisho ya sherehe za Idd el Hajj zilifanyika katika kijiji cha Micheweni Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.
SOURCE:ZanziNews
Maoni
Chapisha Maoni