Siku 29 za Magufuli..

Wakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara
Wakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara wakimsikiliza mgombea mwenza wa urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan alipokuwa akiwahutubia juzi. 


Kigoma. Wakati mgombea urais wa CCM John Magufuli ametimiza siku 29 za kampeni, baadhi ya maeneo aliyopita kuwanadi wagombea ubunge wa chama chake, alikutana na wakati mgumu kwa baadhi ya wabunge kukataliwa na wananchi.
Magufuli ambaye amekampeni mikoa 13 amekuwa akikubalika kwa wananchi wengi wa maeneo aliyopita, alipata wakati mgumu mkoani Kigoma, ambapo wananchi walionyesha wazi kutowakubali wagombea wanne wa ubunge kupitia chama hicho kwa ‘kuwachunia’ kwenye mikutano ya kampeni ya mgombea huyo wa urais.
Kukataliwa kwa wagombea hao wa ubunge kulidhihirika wazi wakati Dk Magufuli akiwatambulisha na kuwaombea kura kwa wananchi, tofauti na ilivyokuwa katika maeneo mengine.
Wagombea hao ni Dk Amani Kabourou wa Kigoma Mjini ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma, Hasna Mwilima wa Kigoma Kusini, Daniel Nsanzugwanko wa Kasulu Mjini na Albert Obama wa Manyovu.
Mkoa wa Kigoma umekuwa ngome ya vyama vya upinzani, ikianza na Chadema miaka 1990, baadaye NCCR-Mageuzi.
Upinzani huo ni mojawapo ya kukataliwa kwa wagombea hao hadharani katika mkoa huo wenye majimbo manane, ambao katika uchaguzi uliopita NCCR-Mageuzi kilishinda majimbo manne ya Kigoma Kusini, Kigoma Kaskazini, Kasulu Mjini na Muhambwe, wakati Chadema ilipata jimbo moja la Kigoma Kaskazini.
Wakati wa ziara ya Dk Magufuli katika Wilaya ya Uvinza, jimbo la Kigoma Kusini, wananchi waliohudhuria mikutano hiyo walionyesha kumkubali zaidi mgombea urais wa CCM kuliko wagombea ubunge.
Septemba 16 wakati Dk Magufuli akihutubia mkutano wa kampeni katika uwanja wa Kawawa, jimbo la Kigoma Mjini ndipo mambo yalipoanzia pale alipomtambulisha Dk Kabourou.
Wananchi walisikika wakisema ‘hapana, hapana, hatukutaki...’ na kuonyesha ishara ya kumkataa mgombea huyo. Hata hivyo, Dk Kabourou hakujali kelele zao na kuendelea kutoa hotuba yake kabla ya kumkaribisha Dk Magufuli.
Mkazi wa Kigoma, Mlenda Nyange alisema wananchi wa Kigoma Mjini hawamtaki Dk Kabourou kwa sababu alikuwa akiwadharau alipokuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia Chadema mwaka 2000 - 2005.
Wakati wa kampeni katika jimbo la Manyovu, Wilaya ya Buhigwe, wananchi hawakuitikia salamu ya mgombea ubunge, Albert Obama kama walivyofanya kwa mgombea urais wakati wote wa hotuba yake.
Jimbo la Kasulu Mjiniwakati Nsanzugwanko akizungumza wananchi walianza kutawanyika na kusikika wakisema, ‘hana jipya huyo...’
Magufuli leo ataendelea na mkutano wa kampeni jimboni kwake Chato.
Wakati huo huo kutoka mkoani Kilimanjaro, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, amewataka wakazi wa Vunjo, mkoani Kilimanjaro, kutofanya makosa ya kuchagua mbunge na madiwani kutoka upinzani ambao hawana sera ambazo zinaweza kuchochea maendeleo yao, badala yake wachague wagombea wa CCM kuanzia rais, wabunge na madiwani.
Kinana aliyasema hayo jana kwenye mkutano wa kampeni za kumnadi mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM, Innocent Shirima, mgombea urais Dk John Magufuli na madiwani wa chama hicho.
Alisema CCM ndiyo chama pekee kinachoweza kuwaletea maendeleo ya haraka, kutatua kero zao mbalimbali na kuongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dk Magufuli, kitafuta sheria kandamizi zinazowaumiza wananchi.
Sheria hizo ni ile ya kuzuia wananchi wasikate miti ambayo wameipanda wenyewe, ili waweze kujikwamua kiuchumi akisema ni jukumu la mbunge na madiwani wa CCM kuhakikisha sheria zote kandamizi zinafutwa.
Kinana alisema inashangaza sheria ya kuzuia kukata miti kuwa na urasimu mwingi ukiwemo wa wananchi kutakiwa kuomba kibali kuanzia ngazi ya kijiji hadi halmashauri na mlolongo mrefu wa kukipata kwake.
Aliwataka wabunge na madiwani ambao watachaguliwa katika uchaguzi ujao, kuhakikisha wanadhibiti michango holela shuleni ili kuleta mabadiliko ya kweli kwa Taifa.
“Serikali imefuta ada katika shule za msingi na sekondari, lakini walimu wamekuwa wakibuni michango mbalimbali kwa maslahi yao binafsi jambo ambalo limekuwa likiwakandamiza wazazi,” alisema.


SOURCE:Mwananchi












 

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

USAJILI WENYE MANUFAA EPL HADI SASA..