Prisons Yazidi Kutakata Ligi Kuu...
PRISONS ‘Wajelajela’leo imeendeleza ubabe wake baada ya kuichapa Mgambo JKT kwa bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu uliopigwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Mchezo huo ulianza kwa timu zote kushambuliana kwa zamu huku Prisons wakipoteza nafasi nyingi za wazi katika kipindi cha kwanza. Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalika milango yote ilionekana kuwa migumu kwani hakuna timu iliyoona lango la mwenzake.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi hasa kwa Prisons, kwani waliliandama lango la wapinzani wao kwa mashuti makali ambayo yaliashiria ushindi katika kipindi hicho. Mohamed Mkopi ndiye aliwainua mashabiki wa Prisons baada kuipatia timu yake goli la kwanza dakika ya 66 baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Meshack Selemani.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mechi hiyo, kocha wa Prisons, Salum Mayanga alisema haikuwa kitu rahisi kwa timu yake kushinda kwani wapinzani wao walikuwa vizuri . “Mechi ya leo haikuwa kitu rahisi kushinda ila wachezaji wangu wameitumia nafasi moja vizuri ingawaji tumepoteza nafasi nyingi.” Kwa upande wake kocha wa Mgambo, Bakari Shime alisema ni moja ya matokeo na wapinzani wao walitumia nafasi walizopata na kuzitumia vizuri. Katika michezo mingine matokeo yalikuwa kama hivi, JKT Ruvu 0 Stand 1, Mtibwa Sugar 1 Majimaji 0, Coastal 0 Mwadui 0.
SOURCE:Sports Starehe
Maoni
Chapisha Maoni