Kenya: walimu waendelea na mgomo licha ya amri ya mahakama..
Shule ya msingi ya Kogelo, magharibi mwa mji wa Nairobi, moja ya shule zinazokabiliwa na mgomo wa walimu.
Mgomo wa walimu umeendelea nchini Kenya, huku shule nyingi zikifungwa licha ya amri ya mahakama ya kuwataka walimu warejee shuleni Jumatatu wiki hii.
Mgomo huu wa walimu nchini Kenya umeingia wiki yake ya tano.Vyama vya walimu vimeapa kutotekeleza amri ya mahakama iliyowataka kusitisha mgomo kwa siku tisini kuanzia Jumatatu wiki hii.
Hata hivyo vyama hivyo vya walimu vimeripoti mahakamani kutaka ufafanuzi zaidi kuhusu uamuzi wa Mahakama wa kuwataka walimu kurejea shuleni. Lakini kesi hiyo imeahirishwa hadi Alhamisi Octoba 1, 2015.
Walimu walijitokeza kwa wingi wakiandamana na viongozi wao wa vyama vya walimu walipojielekeza mahakamani.Walimu walikwenda mahakamani kutafuta ufafanuzi kuhusu ratiba ya mihula ambayo serikali ilibadilisha mgomo uliposhika kasi.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi alhamisi saa nane u nusu kwa sababu jaji aliyekuwa akisikiza kesi hiyo aliomba radhi iliapokee matibabu.Mwanzoni mwa wiki iliyopita, Mahakama Kuu nchini Kenya ilisimamisha agizo la serikali la kutaka shule zote ikiwa ni pamoja na zile za umma au za kibinafsi, zifungwe tangu Jumatatu wiki iliyopita kutokana na mgomo wa waalimu.
Mahakama hiyo ilitoa agizo hilo kufuatia kesi iliyowasilishwa na Chama cha Shule za Kibinafsi kupinga agizo la wizara ya elimu lililotolewa Ijumaa Sepemba 18.
Serikali ilikuwa iliagiza wanafunzi wote kusalia nyumbani Jumatatu Septemba 21isipokuwa wale wanaojiandalia mitihani ya kitaifa.
Hata hivyo mgomo wa walimu unaendelea kushuhudiwa nchini humo, huku ukiathiri mambo mengi ikiwa ni pamoja na kushuka kwa kiwango cha elimu kwa wanafunzi na wengi kwa sasa wamekua wakiranda randa hovyo mitaani.
SOURCE:rFi Kiswahili
Maoni
Chapisha Maoni