Twaweza yawagonganisha watumiaji mitandao ya kijamii....
Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza , Aidan Eyakuze.
Dar es Salaam. Siku moja baada ya Taasisi ya Twaweza kutoa matokeo ya utafiti unaoonyesha kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli anakubalika zaidi kuliko mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa, imeibua mjadala mzito kwenye mitandao ya kijamii kati ya wafuasi wa wagombea hao.
Katika matokeo ya utafiti huo uliofanyika kati ya Agosti na Septemba mwaka huu na kuhoji watu 1,848 yameonyesha kuwa endapo Uchaguzi Mkuu ungefanyika sasa, Dk Magufuli atashinda kwa asilimia 65 dhidi ya Lowassa kwa asilimia 25, ikionyesha tofauti kubwa na utafiti mwingine wa taasisi hiyo uliofanywa Novemba mwaka jana.
Utafiti huo ulionyesha kuwa kama Uchaguzi Mkuu ungefanyika wakati huo, Lowassa angewazidi makada wengine wa CCM, Chadema, NCCR na CUF kwa asilimia 13, wakati Magufuli alikuwa na asilimia 3 tu.
Lakini matokeo yaliyotolewa jana, ikiwa imepita miezi 10, yameonyesha Dk Magufuli anamzidi Lowassa kwa asilimia 40.
Tofauti hiyo pamoja na matokeo ya jumla ya utafiti huo yamezua mjadala huku baadhi ya wadau kuyapinga.
Mjadala huo umeendelea kushika kasi kwenye mitandao ya kijamii hasa kutoka kwa makundi yanayounga mkono wagombea hao wawili wanaoonekana kuchuana vikali kwenye kinyang’anyiro hicho.
Makundi hayo yanapatikana zaidi kwenye mitandao ya kijamii ya Facebook, What’sApp, Twitter na Telegram.
Miongoni mwa makundi ni la ‘Team Lowassa’ ambalo baada ya matokeo hayo, jana liliweka nukuu mbalimbali za baadhi ya viongozi mbalimbali duniani kama aliyewahi kuwa waziri mkuu wa Uingereza, Winston Churchill ambaye aliwahi kusema “Takwimu pekee za kuziamini ni zile tu unazoweza kuzithibitisha mwenyewe.”
Kundi hilo ambalo lilikuwa na wafuasi 244,157 hadi jana, liliweka nukuu nyingine ya aliyekuwa waziri mkuu baada ya Churchill, Benjamin Disraeli ambaye alisema: “Takwimu ni uongo, uongo na uongo.”
Kundi hilo lenye kauli mbiu, ‘Sauti ya wengi, Sauti ya Mungu’, baada ya kuweka nukuu hizo baadhi wafuasi waliendelea kuhoji uhalali wa utafiti huo.
Mmoja wa wafuasi hao aliyetumia jina la Deus Charles alihoji, “Turudi katika sampuli tume ya Warioba (Joseph), alihoji watu 48, 000. Kati ya hao 17, 000 ndio waliozungumzia mambo ya Muungano na walitaka serikali tatu,”alihoji Charles.
“CCM wakasema idadi hiyo ni ndogo sana kuwakilisha maoni ya Watanzania. Sasa iweje watu 1848 watusemee wapiga kura zaidi ya milioni 20?”
Mfuasi mwingine wa timu hiyo aliyetumia jina la Success Kilian alisema, “Team Lowassa naomba muwaulize (Twaweza) utafiti ulifanyika mwezi wa nane, je mazingira ya kisiasa ya wakati huo na sasa si sawa?.”
“…Wakati huo Lowassa alikuwa CCM ndiyo maana walikuwa na uhakika wa kushinda ila kwa sababu hivi sasa yupo Chadema mambo yamegeuka.”
Wakati ‘Team Lowassa’ wakipinga matokeo ya utafiti huo, ‘Team Magufuli’ waliweka picha nane zenye takwimu ya matokeo ya utafiti wa Twaweza na kuandika ujumbe katika ukurasa wake wa Facebook , uliosoma“#Hapakazi tu…Matokeo ya tafiti ya Twaweza Dk Magufuli azidi kuongoza.”
Katika ukurasa huo uliokuwa na wafuasi 7,212 hadi jana baadhi ya wafuasi akiwamo, Masanja Samora aliandika ujumbe uliosoma, “Magufuli oyeeee wataisoma namba.”
Mfuasi mwingine aliyetumia jina la Aishay Msumi kwenye ukurasa huo, alisema huo ni mwanzo tu, CCM mbele kwa mbele.
Pongezi hizo ziliendelea kutolewa na wafuasi wa kundi lililopewa jina la ‘Team Magufuli, Community’ lililokuwa na wafuasi 1,929 hadi jana huku baadhi ya wafuasi wakisema Dk Magufuli ndiyo habari ya mjini.
Mtumaji wa akaunti ya Twitter, Papaa Mchoyo @salimi_alkhasas alisema, “Utafiti huu hatujatazama sana asilimia, tunazijua. Tumejifunza zaidi turekebishe vitu gani kwa wananchi.
Mtumiaji huyo alisema kazi kubwa inayofanywa na Dk Magufuli na Mama Samia (Suluhu, mgombea mwenza) inafanya CCM iendelee kupanda zaidi.
Maoni
Chapisha Maoni