EU yatuma kikosi cha waangalizi 140 wa uchaguzi..



Umoja wa Ulaya (EU) umetuma kikosi cha watu takriban 140 watakaofanya uangalizi wa mwenendo wa Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika siku 23 zijazo.

 Waangalizi hao wanaojumuisha wataalamu mbalimbali wa masuala ya uchaguzi, wanasiasa, baadhi ya maofisa kutoka balozi za nchi za EU nchini, na waangalizi waliajiriwa kutoka Tanzania, watakuwemo nchini hadi mchakato wa uchaguzi utakapokamilika.

 Mkuu wa kikosi cha uangalizi cha EU, (EU EOM), Judith Sargentin amewaambia wanahabari leo kuwa kikosi hicho kitakuwa na kazi kuu ya kuangalia iwapo uchaguzi utafanyika kwa kufuata misingi, sheria na kanuni za nchi, za kikanda na zile za kimataifa kama misingi ya kujenga demokrasia.

 Amesema tayari baadhi ya waangalizi walishaanza kuwasili nchini mwanzoni mwa Septemba ikiwemo timu ya wataalamu wa masuala ya siasa, uchaguzi na sheria zinazohusiana na mchakato wa uchaguzi iliyowasili nchini Septemba 11.

 “Katika kipindi chote cha uangalizi tutakuwa huru, hatutafungamana na upande wowote na mwishoni tutatoa ripoti ambayo itakuwa na mapendekezo ya kusaidia maboresho ya chaguzi zijazo,” amesema Sargentin ambaye pia ni mbunge kutoka Uholanzi.

 “Tutafanya kazi kwa weledi kwa kufuata viwango na taratibu zinazokubalika kimataifa na Umoja wa Ulaya. Waangalizi wetu wanazingatia kanuni za maadili kwa wangalizi wa chaguzi za kimataifa zinazoambatana na tamko la Kimataifa la kanuni za uangalizi wa uchaguzi la mwaka 2005.”

 Amesema kundi la waangalizi wa muda mrefu 34 walishasambazwa kwenye vituo vya uangalizi tangu tarehe 27 mwezi huu kuangalia maandalizi yote ya uchaguzi bara na visiwani.

 Ameeleza kuwa tayari kundi la waangalizi hao wa muda mrefu limeanza kukutana na maofisa wa uchaguzi, wagombea na wawakilishi wa asasi za kiraia na watatuma ripoti ya watakayoyaona kwa kundi kuu jijini hapa ili watoe tathmini ya kina isiyo na upendeleo.


 Moja ya mambo ambayo waangalizi hao watayaangalia ni uhuru wa vyama vya siasa kufanya mikutano yao pasipo bugudha na kuvunja sheria, ufanisi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), uhuru wa wananchi kushiriki kwenye mchakato huo na upigaji kura na namna vyombo vya habari vinavyoripoti vyama na wagombea.






SOURCE:Muungwana Blog

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

USAJILI WENYE MANUFAA EPL HADI SASA..