Maalim Seif kuviunda upya vikosi vyua Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar endapo atapata ridhaa ya wananchi...
Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwahutubia wafuasi wa chama hicho katika viwanja vya Mkele Zanzibar.
Wafuasi wa CUF wakimsikiliza mgombea wao wa Urais katika viwanja vya Mkele Zanzibar.
Wafuasi wa CUF wakimsikiliza mgombea wao wa Urais katika viwanja vya Mkele Zanzibar.
Mkurugenzi wa mawasiliano wa Timu ya Ushindi (CUF) Ismail Jussa Ladhu akiwahutubia wafuasi wa chama hicho katika viwanja vya Mkele Zanzibar.
Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akimkabidhi kadi ya CUF mmoja kati ya wanachama wapya waliojiunga na Chama hicho wakitokea CCM kutoka majimbo ya Kwahani na Shaurimoyo.
Bi. Fat-hiya Salim akitoa salamu za wanawake katika mkutano wa kampeni za CUF uliofanyika viwanja vya Mkele.Wafuasi wa CUF wakiwa makini kusikiliza kampeni za mgombea Urais katika viwanja vya Mkele Zanzibar.
Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesema iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar ataviunda upya vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuvipatia vitendea kazi na kuimarisha maslahi yao.
Amesema vikosi hivyo viliundwa kwa malengo maalum lakini bado havijatimiza malengo yake kutokana na mazingira duni ya kazi zao, jambo ambalo amesema katika uongozi wake atavijengea mazingira bora ili vifanye kazi kwa ufanisi.
Maalim Seif ameeleza hayo katika viwanja vya Mkele mjini Zanzibar, wakati akihutubia mkutano wa kampeni kwa ajili ya majimbo ya Kwahani na Shaurimoyo.
Amesema vikosi vyote vikiwemo KMKM, JKU, KVZ, Zimamoto na Chuo Cha Mafunzo, vitapatiwa vitendea kazi vya kisasa pamoja na kurekebisha mishahara na maposho yao, ili viweze kulingana na vikosi vya Muungano.
Akizungumzia kikosi cha KMKM, Maalim Seif amesema atakibadilisha jina na kukiita kikosi cha ulinzi wa bahari, na kukipatia zana zote zinazohitajika katika utendaji wao, ili kiweze kufuatilia pia usalama wa wananchi wanapokuwa baharini.
Kuhusu Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), Maalim Seif amesema mbali ya kuliwekea maslahi bora na vitendea kazi vya kisasa, pia ataliwekea mazingira ya kutoa utaalamu wa fani mbali mbali kwa vijana, ili watakapomaliza mafunzo yao waweze kujiajiri.
Amefahamisha kuwa kikosi cha zimamoto na uokozi kwa upande wake kitapatiwa zana za kutosha za uokozi pamoja na magari ya kuzimia moto ili kuweza kukabiliana vyema na majanga yanapotokea.
Mapema akitoa salamu za wanawake wa majimbo hayo, Bi Fat-hiya Salim, amewashauri wanawake kumchagua Maalim Seif ili aweze kutatua changamoto zinazowakabili zikiwemo huduma za afya.
Amesema kwa muda mrefu wanawake wamekuwa wakihangaikia huduma hizo huku wakikabiliwa na mazingira magumu ya kimaisha, na kwamba iwapo watamchagua Maalim Seif ataweza kutatua changamoto hizo kwa kupatiwa huduma hizo bila ya malipo.
Nae kijana Othmani Haji amesema bado vijana wengi wanashindwa kujitokeza hadharani kutokana na kuwaogopa wazazi wao ambao hawajataka kubadilika, lakini watakipigia kura chama cha CUF.
Ameelezea kufurahishwa na jinsi vijana wa majimbo hayo walivyohamasika kukiunga mkono Chama hicho na kutetea maslahi ya nchi yao, baada ya kutembelea barza saba za chama hicho katika majimbo hayo.
Katika mkutano huo Maalim Seif amekabidhi kadi kwa wanachama wapya 26 kutoka majimbo ya Kwahani na Shaurimoyo ambao wamekihama Chama Cha Mapinduzi na kujiunga na CUF.
Chama hicho kimesimamisha kampeni zake kupisha sherehe za sikukuu ya Eid El-Hajj zinazoanza tarehe 24/09/2015, ambapo amesema baada ya hapo kitatangaza maslahi kamili ya wafanyakazi na vikosi vya SMZ.
SOURCE:ZanziNews
Maoni
Chapisha Maoni