Tofauti za sheria EAC zinavyovuruga utekelezaji wa maazimio...



Tunaweza kuwa na maazimio mazuri yanayolenga kuharakisha maendeleo miongoni mwa wanachama, lakini kama yanakinzana na taratibu walizojiweka watu, inakuwa kama mtu anayetwanga maji kwenye kinu akitarajia atapata unga
Miongoni mwa madhumuni ya kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni kukuza uchumi na maendeleo endelevu kwa kuhimiza uendelezaji wa uchumi kwa nchi wanachama.
Hayo yamepangwa kufanyika kwa uwiano sawa wa maendeleo ya kiuchumi unaoweza kuinua hali ya maisha ya jamii, matumizi endelevu ya maliasili na kuchukua hatua za utunzaji wa mazingira.
Madhumuni mengine ni kuimarisha ushirikiano wa kihistoria wa kiuchumi, kijamii na kisiasa uliojengeka kwa muda mrefu ili kuhimiza maendeleo ya watu wake katika nchi zote wanachama wa EAC, Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda.
Mambo mengine yanayojumuishwa kwenye madhumuni hayo ni masuala ya jinsi, maendeleo ya kiteknolojia, kuendeleza amani, usalama, ujirani mwema, kuimarisha ubia wa sekta ya umma na binafsi kwa maendeleo endelevu ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Hatua za mtangamano kimaendeleo
Ili kudumisha madhumuni ya EAC, Ibara ya 5 (2) ya Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki inaeleza kuwa: Nchi Wanachama zitaanzisha Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja, kisha Umoja wa Fedha na hatimaye Shirikisho la Kisiasa.
Lengo la Umoja wa Forodha ni kuondoa ushuru wa forodha na vikwazo visivyo vya kiforodha kwa biashara ya bidhaa zinazozalishwa miongoni mwao na kukidhi vigezo vya uasili wa bidhaa. Soko la pamoja kuunganisha masoko yao ya bidhaa huduma, ajira na mitaji na hivyo kuunda soko moja kubwa lisilo na vikwazo miongoni mwao.
Umoja wa Fedha inalenga kujenga sera moja ya fedha na kutumia sarafu moja katika kuimarisha soko la pamoja.
Shirikisho la kisiasa litasaidia kuunganisha nchi zote na kuwa taifa moja. Nchi zote zitakubaliana kuunganisha nchi zao na kuwa nchi moja, himaya moja ya utawala wa kisiasa.

Mafanikio
Baadhi ya maeneo ya mikakati ya EAC, yanayoonekana kufanikiwa ni utekelezaji wa mfumo wa biashara unaofanana, Umoja wa Forodha, uwekezaji na maendeleo ya viwanda, ushirikiano katika maendeleo ya viwanda, uoanishaji wa sera na taratibu za uwekezaji, uendelezaji wa utafiti na maendeleo ya viwanda na kuendeleza uhusiano wa kiuzalishaji baina ya viwanda.

Kinachokwamisha malengo
Wataalamu wa mambo ya uchumi waliokutana jijini Dar es Salaam hivi karibuni na kujadili kwa kina maazimio mbalimbali ya EAC wakitafiti ni kwa nini baadhi ya mipango inayopangwa haitekelezwi.
Katika mjadala huo, ilibainika kuwa tofauti za sheria zinazosimamia biashara katika nchi za Afrika Mashariki, zinakwamisha kufikiwa kwa malengo hayo.
Seneta wa Kisumu nchini Kenya, Profesa Peter Anyang Nyong’o anasema hivi sasa zipo baadhi ya sheria ambazo zimekuwa kikwazo kwa wafanyabiashara kutoka Kenya kuingiza bidhaa zao nchini.
“Kwa sababu ikiwa tunatofautiana katika sheria wafanyabiashara hawawezi kufanya biashara kuvuka mpaka, kwa hiyo lazima kuwepo na uhusiano sawasawa kati ya sheria inayotumika huko Nairobi na hapa Dar es Salaam,” anasema Profesa Nyong’o.
Ngong’o ambaye amewahi kuwa Waziri wa Afya wa Kenya, anasema kutokana na tofauti hiyo ya kisheria, baadhi ya raia wa Kenya akiwamo binti yake wameshindwa kupata kazi hapa nchini huku Watanzania nao wakikutana na changamoto kama hiyo nchini Kenya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa, Profesa Samuel Wangwe anasema kuwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zimekuwa zikikubaliana kisiasa kuwa jumuiya, hata hivyo kuna mambo kadhaa ambayo hayatekelezwi.
“Tumekutana mara hii kwa sababu tunaamini kuna mambo mengi ambayo hatujayaelewa vizuri tunazungumzia ili sasa tupange namna ya kuanza kuyafanyia utafiti tuyaweke vizuri zaidi,” anasema Profesa Wangwe.
Anaeleza kuwa utafiti huo utalenga katika kuangalia nafasi ya biashara na sekta binafsi katika kuwezesha uchumi wa Jumuiya hiyo kukua haraka na kwamba tayari walishakubaliana kubadilishwa kwa sheria mbalimbali zinazoonekana kuwa vikwazo kwa maendeleo ya nchi husika.
“Lakini kubadilisha sheria kumekuwa taratibu sana, ndio tunataka tujue kwa nini?” anahoji.
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Profesa Joseph Semboja anasema wafanyabiashara wa Tanzania wanaofanya biashara Kenya na Uganda wanapata matatizo na wakati mwingine wanaziona fursa kwa hiyo usipowashirikisha kwenye kuzungumzia masuala haya utakuwa umeacha sehemu kubwa ya ushirikiano wa kikanda.


SOURCE:Mwananchi


















Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

USAJILI WENYE MANUFAA EPL HADI SASA..