Yanga yasema imetosha, yailaza Simba Taifa..

Mashabiki wa Yanga wakishangilia ushindi wa
Mashabiki wa Yanga wakishangilia ushindi wa timu yao baada ya kufanikiwa kuilaza Simba katika mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara uliochezwa kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam leo. 

Dar es Salaam. Kama kuna mtu atakayekuwa na furaha leo kati ya wachezaji wa Yanga bila shaka atakuwa mshambuliaji, Malimi Busungu ambaye ameisaidia timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wapinzani wao wa jadi Simba.
Busungu atakuwa na furaha baada ya kutoa pasi kwa Amissi Tambwe katika dakika ya 44 ambaye hakufanya ajizi zaidi ya kuukwamisha kimiani kwa shuti na kuiandikia Yanga bao la kuongoza.
 Bao hilo liliamsha shangwe, nderemo na vifijo toka kwa mashabiki wa wanajangwani hao waliojazana kwenye uwanja wa Taifa wenye uwezo wa kubeba mashabiki 60,000 walioketi.
Hadi mapumziko Yanga walikuwa wanaongoza kwa bao 1-0.
Bao la pili la Yanga lilifungwa na Malimi Busungu mwenyewe katika dakika ya 79 akiunganisha kimiani kwa kichwa mpira uliorushwa na kiraka Mbuyu Twite ambao hata hivyo beki wa Simba, Hassan Isihaka alijaribu kuuokoa.
Hata hivyo, mchezo huo haukuvutia sana kama wengi walivyotarajia badala yake ulitawaliwa na butuabutua nyingi na rafu zilizotokana na kukamiana kwa wachezaji wa timu zote hali iliyomfanya mwamuzi kutoa kadi za njano kwa wachezaji kadhaa wa timu zote.
Miongozi mwa walioonyeshwa kadi za njano katika mchezo huo ni mabeki Juuko Murshid na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na Mussa Hassan ‘Mgosi’ wa Simba huku kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ akionyeshwa kwa upande wa Yanga.
Kiraka Mbuyu Twite wa Yanga alionyeshwa kadi nyekundu dakika za majeruhi baada ya kuchelewa kurusha mpira. Ilikuwa ni kadi ya pili ya njano kufuatia awali kuonywa kwa kadi ya njano kutokana na mchezo usio wa kiungwana.
Kwa matokeo hayo, Yanga inazidi kujikita kileleni baada ya kujikusanyia pointi 12 na mabao 11 ya kufunga huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara moja tu.
Vikosi vya timu hizo vilikuwa hivi:
Simba: Manyika Peter, Hassan Kessy, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka, Juuko Murshid, Justice Majabvi, Said Ndemla, Mwinyi Kazimoto, Mussa Hassan ‘Mgosi’, Hamis Kiiza na Awadh Juma.
Yanga: Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Haji Mwinyi, Nadir Haroub, Kelvin Yondani, Thabani Kamusoko, Simon Msuva, Salumu Telela, Amissi Tambwe, Donald Ngoma na Haruna Niyonzima.
Matokeo mengine katika mechi za mfululizo wa ligi hiyo yalikuwa hivi: JKT Ruvu 0-1 Stand United; Mtibwa Sugar 1-0 Majimaji; Coastal Union 0-0 Mwadui; Prisons 1-0 Mgambo na Kagera Sugar 0-0 Toto Africans.


SOURCE:Mwananchi
  























































Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

USAJILI WENYE MANUFAA EPL HADI SASA..