Bomoabomoa yaacha vilio, simanzi Dar...
Vijana wakihamisha mabaki ya vitu vilivyosalia baada ya kubomolewa kwa vibanda vya biashara na nyumba zilizokuwa katika hifadhi ya barabara eneo la Mwenge karibu na Maghorofa ya Jeshi jijini Dar es Salaam jana.
Dar es Salaam. Manispaa ya Kinondoni jana ilisababisha vilio kwa wakazi wa maeneo wa wilaya hiyo ilipoanza ubomoaji wa nyumba zilizojengwa maeneo ya wazi na hifadhi kinyume cha sheria. Juzi, Kamishna wa Ardhi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Moses Kusirika alitangaza operesheni ya kubomoa nyumba hizo kuanzia jana na kuwa baada ya Kinondoni watahamia wilaya nyingine na mikoani pia.
Miongoni mwa maeneo yaliyokumbwa na bomoabomoa hiyo jana ni Mwenge, Sinza, Biafra-Bwawani na Mivumoni.
Mwenge
Ubomoaji katika mtaa wa TRA Mwenge, ulianza saa 10 alfajiri, ambapo nyumba za biashara na makazi 15 zilibomolewa chini ya ulinzi mkali wa polisi.
Huku baadhi wakiangua vilio, wakazi waliokumbwa na hatua hiyo walilalamika wakidai hawakuwa na taarifa za kuwapo kwa ubomoaji huo, jambo lililosababisha baadhi yao kushindwa kuokoa mali zilizokuwa ndani.
Mwananchi ilishuhudia baadhi ya vijana wakitumia kaulimbiu iliyoanzishwa na Rais John Magufuli ya ‘Hapa kazi tu’ huku wengine wakiimba nyimbo kuwa ‘Mliichagua wenyewe, Serikali ni ileile’ wakati ubomoaji huo ukiendelea eneo la Mwenge.
Akizungumza na Mwananchi, mmoja wa wamiliki wa nyumba zilizobomolewa katika eneo hilo, Atupokile Mwakasile (70) alidai hana mahali pa kwenda kwa kuwa nyumba yake ilijengwa tangu mwaka 1984, baada ya kupewa kiwanja hicho na ushirika.
Aliongeza kuwa tangu afiwe na mumewe mwaka 2006, nyumba hiyo iliyokuwa na wapangaji wanne ndiyo ilikuwa ikimuingizia kipato ambacho kilimsaidia kimaisha na familia yake.
“Leo (jana) naona dalili za kulala nje na familia yangu kwa kuwa sina mahali pa kwenda. Kibaya zaidi sijaweza kuokoa kitu chochote, vitu vyote vimeharibiwa baada ya nyumba kubomolewa,” alisema Mwakasile.
Kwa upande wake, mfanyabiashara wa eneo hilo, Norasco Shirima (34) alisema ubomoaji huo umemsababishia hasara ya zaidi ya Sh14 milioni.
“Nina miezi minane tu tangu nikarabati jengo hili kwa ajili ya biashara yangu ya vinywaji, japo nilikuwa mpangaji, cha ajabu ni hata mwenye nyumba hakuwahi kuniambia kama siku moja tutabomolewa,” alisema Shirima.
Mfanyabishara wa Samaki, katika eneo la Mwenge, Ramla Abdallah alisema ubomoaj huo umemsababishia hasara ya Sh5 milioni, alizodai amekopa benki.
Sinza
Msimamizi wa ubomoaji katika eneo la Sinza E, Baraka Mkuya alisema eneo hilo lilikuwa la wazi, lakini lilifanywa gereji.
Mkuya ambaye ni mhandisi wa Manispaa ya Kinondoni, alisema wameamua kuvunja vibanda vya gereji hizo na kuwataka wahusika waachie eneo hilo kwa shughuli zitakazopangwa.
“Hawa tuliwafukuza kipindi cha nyuma na tulishawaeleza kuwa eneo hili ni la wazi lakini nashangaa kuona wamerudi tena.
“Baada ya kubomoa tutawaletea stakabadhi za malipo, ili walipe gharama za manispaa kubomoa eneo hili kwa mara nyingine kwa kuwa walishakatazwa,” alisema Baraka.
Aliwataka wananchi waliovamia maeneo yasiyoruhusiwa na kujenga makazi yao kuondoka mara moja kabla hawajabomolewa nyumba zao.
Mmoja wa mafundi gereji wa Mtaa wa Sinza E, aliyejitambulisha kwa jina moja la Omary, alisema kabla ya ubomoaji walipewa taarifa, hivyo operesheni imefanyika kihalali na imefuata taratibu.
Biafra- Bwawani
Katika eneo la Biafra-Bwawani, nyumba moja iliyodaiwa kuwa na mgogoro wa muda mrefu ilibomolewa huku mmiliki wa nyumba hiyo akifanikiwa kuhamisha mali zote isipokuwa ng’ombe, waliokabidhiwa kwa uongozi wa mtaa.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, Mohamed Mkanda (CUF) alisema uamuzi wa manispaa kubomoa nyumba hiyo umewafanya wananchi wa eneo hilo kuamini ahadi za Rais Magufuli, za kutowafumbia macho wanaovunja sheria.
Katika eneo la Mivumoni, Mbezi, Mkuya alisema ilibolewa nyumba moja ambayo imethibitika mahakamani kuwa mmiliki wake aliijenga kwenye kiwanja cha mtu mwingine.
Imeandikwa na Tumaini Msowoya, Bakari Kiango na Salma Nganogera
Maoni
Chapisha Maoni