Lowassa, Maalim Seif wateta kwa dakika 90...
Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu kikao chao cha faragha kilichoongozwa na Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa (kulia).
Dar es Salaam. Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa jana alifanya mazungumzo ya takriban saa moja na nusu na mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kuhusu hali ya sintofahamu ya Zanzibar iliyosababishwa na kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu wa visiwa hivyo.
Dar es Salaam. Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa jana alifanya mazungumzo ya takriban saa moja na nusu na mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kuhusu hali ya sintofahamu ya Zanzibar iliyosababishwa na kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu wa visiwa hivyo.
Kikao hicho kilifanyika katika ofisi ya Lowassa iliyopo Mikocheni, Dar es Salaam kwa dakika 90 kuanzia saa 10:45 hadi saa 12:15 jioni, kikiwahusisha viongozi wakuu wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambavyo ni Chadema, NLD, NCCR-Mageuzi na CUF.
Hata hivyo, viongozi hao hawakutaka kuweka bayana walichozungumza, lakini Maalim Seif akawaeleza wanahabari kwamba kesho, Lowassa atatoa ufafanuzi wa kina kuhusu walichojadiliana.
Waliokuwepo katika kikao hicho ni mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi na mbunge mteule wa Vunjo, James Mbatia, makamu mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari na mjumbe wa kamati kuu wa chama hicho, Profesa Mwesiga Baregu, kaimu mwenyekiti wa CUF, Twaha Taslima na katibu mkuu wa NLD, Tozi Matwange.
Mazungumzo hayo yamefanyika wakati majadiliano ya kina yakiendelea visiwani Zanzibar katika kutafuta muafaka, huku hali ikizidi kuwa ya sintofahamu baada ya kutolewa tangazo kwenye Gazeti la Serikali la kufuta rasmi uchaguzi huo.
Katika hali ambayo haikuwa imetarajiwa, mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Said Jecha alitangaza kufuta matokeo ya kura za Rais wa Zanzibar na wajumbe wa baraza la wawakilishi Agosti 28, akisema mmoja wa wagombea urais alijitangaza mshindi na kwamba kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa sheria na kanuni za uchaguzi.
Hata hivyo, uamuzi wake umepingwa na CUF ambayo imesema Jecha hana mamlaka hayo na pia hakushirikisha wajumbe wengine wa ZEC kabla ya kufikia uamuzi huo, na chama hicho kimeshaweka bayana kuwa hakitambui marudio ya uchaguzi.
Jana, mara baada ya kumaliza kikao hicho, Maalim Seif aliyefika eneo hilo na msafara wa magari manne, alisema: “Kama alivyosema Lowassa atafanya mkutano na waandishi wa habari Jumapili (kesho) saa 5:00 asubuhi, kwa hivyo maelezo yote mtapata hapo.”
Alipotakiwa kueleza msimamo wa chama chake kuhusu hali ya Zanzibar, Maalim Seif alisema: “Msimamo wa CUF upo wazi, hatuoni sababu ya kushiriki tena uchaguzi. Tangazo la (Jecha) mwenyekiti sisi tunaliona si halali kwa sababu uchaguzi haujafutwa.
“Tushiriki (tena uchaguzi) kwa sababu gani. Hatuwezi kwa sababu tumeshiriki uchaguzi huru wenzetu hawataki tuna uhakika gani kama huu mwingine watakubali (kushindwa).”
Alipotakiwa kueleza kinachoendelea katika mazungumzo kati yake na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na marais wastaafu wa pande mbili za Muungano, katibu huyo wa CUF alisema hawezi kulitolea ufafanuzi wowote suala hilo kwa maelezo kuwa muda wa kufanya hivyo bado haujafika.
“Mazungumzo na Shein, hayo wakati wake bado. Mtapata yote wakati wake ukifika,” alisema.
Akizungumzia tangazo la kufutwa kwa uchaguzi Zanzibar lililochapishwa katika gazeti la Serikali, Maalim Seif alisema msimamo unaendelea kuwa ule ule.
“Hata ukisoma tangazo la serikali linasema mimi Salum Jescha nimefuta uchaguzi, na si Serikali. Naona tangazo ni lile lile tu,” alisema Maalim Seif ambaye ameshagombea urais wa Zanzibar mara tano tangu kurejeshwa kwa siasa za vyama vingi mwaka 1992.
Maalim Seif, ambaye alikuwa kada wa CCM kabla ya kujiunga na CUF, hakutaka kuzungumzia maoni ya watu kwamba kutangazwe hali ya hatari visiwani Zanzibar.
“Hayo tuyaacheni sidhani kama imefika huko,” alisema Seif ambaye mwaka huu amekuwa akisisitiza wafuasi wa CUF kuwa watulivu kwa kipindi chote cha uchaguzi.
Lowassa aliingilia sehemu hiyo na kuwataka wanahabari kumuuliza Rais John Magufuli, akisema ndiye atakuwa na majibu sahihi.
Awali, Lowassa alisema kuwa mazungumzo yao yalikuwa na mafanikio na kusisitiza kuwa Jumapili ataeleza walichojadili.
Visiwani Zanzibar, CUF imesema haitambui tamko la Gazeti la Serikali la kurasimisha kufutwa kwa uchaguzi.
Uamuzi wa kufutwa rasmi kwa matokeo ya uchaguzi umetangazwa rasmi katika Gazeti la Serikali la Novemba 6, mwaka huu.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, uamuzi huo umechapwa chini ya kifungu Namba 119 (10) na Sheria ya Uchaguzi Namba 11 ya 1984.
Gazeti hilo pia limetolewa kwa kuzingatia kifungu cha 3(1) na 5(a) vya Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar na kuelezea kuwa matokeo yote ya Uchaguzi Mkuu yamefutwa kuanzia Oktoba 25.
Kifungu cha 3 (1) cha Sheria ya Uchaguzi kinasema: “Kanuni, maelezo na matangazo yote ambayo Tume ina mamlaka ya kutunga au kutoa, itajaliwa kuwa yametungwa au yametolewa kisheria kama yametiwa sahihi na mwenyekiti wa Tume au Mkurugenzi wa Uchaguzi.”
“Mimi Jecha Salim Jecha, mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 119 (10) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na kwa mujibu wa vifungu vya 391) na 5 (a) vya Sheria ya Uchaguzi namba 11 ya mwaka 1984, natangaza uamuzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kufuta matokeo yote ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa tarehe 25, Oktoba,” gazeti hilo la serikali linaeleza.
Tangazo hilo limetiwa saini na mwenyekiti huyo wa ZEC, Oktoba 28 mwaka huu na kwa msingi huo wananchi wa Zanzibar watatakiwa kuingia tena katika uchaguzi ndani ya siku 90.
Akizungumzia tamko hilo, kaimu mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma wa CUF, Ismail Jussa alisema “kimsingi ni kuzidi kujianika mbele ya umma na mbele ya wanasheria kuwa ZEC haikuwa na mamlaka ya kufuta na vivyo hivyo ni kubainisha kuwa Gazeti la Serikali haliwezi kuigeuza haramu kuwa halali, kwa kuwa hata hivyo vifungu vilivyonukuliwa na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar havitoi mamlaka hiyo na ni aibu”.
Maalim akutana na mabalozi
Siku mmoja baada ya Jamii ya Kimataifa kueleza utayari wao wa kusaidia utatuzi wa mgogoro wa kisiasa visiwani, Maalim Seif Sharif Hamad amefanya mazungumzo na wanadiplomasia jijini Dara es Salaam.
Mazungumzo yalifanyika kwa nyakati tofauti kati ya Maalim Seif na mabalozi na wawakilishi wa jumuiya za kimataifa nchini.
Alikutana kwa takriban saa moja na balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) anayemaliza muda wake, Filiberto Sebregondi kwenye Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.
Balozi Sebregondi katika kikao hicho aliongozana pia na ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi kutoka EU na makamu mkuu wa waangalizi, Tania Marques.
Kikao hicho, ambacho si mara ya kwanza kuwakutanisha baadhi ya wanadiplomasia wa EU na Maalim Seif, kilimuhusisha pia naibu katibu mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui na Jussa.
Jussa alisema jana kuwa kikao cha Maalim na mabalozi kilijadili mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar tangu Jecha atangaze kufuta uchaguzi.
Jussa alisema pia kuwa Maalimu alitumia nafasi hiyo kuagana na mwanadiplomasia huyo baada ya kumaliza muda wa utumishi wake nchini.
Melecela amtetea Jecha
Wakati hayo yakiendelea, Waziri Mkuu wa zamani, John Malecela amemkingia kifua Jecha kwa kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar, akisema ndiye mwenye uamuzi wa mwisho ambao hauwezi kubadilika hata kama unapingwa wananchi na jumuiya za kimataifa.
Makamu Mwenyekiti huyo mstaafu wa CCM-Bara aliufananisha uamuzi wa Jecha na refa wa mpira wa miguu, akisema goli ni lazima liwe goli hata kama “litakuwa bao la mkono”.
Akizungumza katika mahojiano na kituo cha redio cha Deutsche Welle (DW) ya Ujerumani jana mchana, Malecela alisema kwa mujibu wa sheria za uchaguzi na Katiba ya nchi, mwenyekiti wa ZEC au wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ndiyo wenye jukumu la kutangaza matokeo ya urais, ambayo hayawezi kupingwa mahakamani.
Alisema imani yake ni kwamba mvutano huo utamalizwa kwa mazungumzo ya amani, kusisitiza kwamba Zanzibar imekuwa na historia ya mapambano kati ya vyama vya CUF na CCM kila unapofanyika uchaguzi mkuu.
“Kwanza ni lazima ujue sheria. Nadhani sheria ya ZEC na NEC zinafanana, zinampa madaraka makubwa mwenyekiti. Mfano akishatoa matokeo ya rais yanakuwa mwisho hayatahojiwa na mtu yeyote katika mahakama,” alisema Malecela, ambaye amewahi kuenguliwa mara mbili kwenye mbio za urais ndani ya CCM kabla ya kufikishwa mbele ya wajumbe kupigiwa kura.
“Nina hakika Jesha alitoa hukumu hiyo akijua anayo madaraka hayo na alitoa sababu. Sitaki kuzungumzia habari za Jecha kutangaza mwenyewe matokeo bila kuwashirikisha wajumbe wengine wa Tume hiyo maana hayo ni mambo yanayosemwa na watu tu,” alisema.
SOURCE:Mwananchi
Maoni
Chapisha Maoni