JK aibukia Addis awapa neno Kili Stars..
Awassa, Ethiopia. Wiki chache baada ya kung’atuka madarakani, Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete ameibukia mjini Addis Ababa, Ethiopia kunakofanyika mashindano ya Kombe la Chalenji huku akiwatakia kila la heri Kilimanjaro Stars.
Kikwete ambaye amejinasibu kuwa shabiki mkubwa wa soka, amewataka Kili Stars wafanye vizuri zaidi na kutwaa taji.
Kilimanjaro Stars ipo mjini Awassa ikishiriki mashindano hayo ya 38 ya Chalenji ikiongoza Kundi A kwa pointi sita.
Kikwete aliyekuwa Ethiopia kuhudhuria mkutano ambao haujafahamika, aliwapigia simu Stars akidhani wapo Addis Ababa ili afike kuwaona, lakini kikosi hicho kipo Awassa, kilometa zaidi ya 300.
Makamu Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia alisema kiongozi huyo mstaafu wa Tanzania alitaka kuona timu na kuiongezea hamasa kutokana na mafanikio ambayo imeyapata hadi sasa.
Karia alisema Kikwete aliwapigia na kuzungumza nao mambo kadhaa, ikiwamo kuwapongeza kwa kufuzu kucheza robo fainali ya mashindano hayo, akiwataka waongeze bidii na kutodharau timu yoyote.
“Tulizungumza na Kikwete na alitupongeza kwa mafanikio haya, lakini zaidi alitaka kuja baada ya kumaliza shughuli zake mjini Addis Ababa, alijua tupo mji humo, lakini kwa bahati mbaya alitakiwa kurudi Tanzania leo (jana).
“Kikubwa, ametutaka tusidharau timu yoyote katika mashindano haya na tuwe na umakini katika kuhakikisha tunarudi na taji nyumbani,” alisema Karia.
Kibadeni na kiu ya Watanzania
Kocha wa Kili Stars, Abdallah Kibaden ‘ King’ alisema Watanzania wamemtuma ubingwa, hivyo atacheza kwa nguvu katika michezo yote licha ya kufuzu kwa hatua ya robo fainali.
Ushindi wa juzi dhidi ya Rwanda wa mabao 2-1 katika mashindano ya Kombe la Chalenji uliihakikishia Stars kusonga mbele katika hatua ya robo fainali baada ya kushinda mechi zake mbili kati ya tatu.
Kilimanjaro Stars, inaongoza Kundi A lenye timu za Ethiopia, Rwanda na Somalia, ikiwa na pointi sita, ambazo haziwezi kufikiwa na yeyote hadi leo, kwani mechi za jana za kundi hilo zilikutanisha timu zilizofungwa katika michezo yao ya kwanza (Ethiopia na Somalia).
Akizungumza mara baada ya kuibuka na ushindi huo muhimu, Kibaden alisema anaamini kuwa atatimiza malengo yake na kukata kiu ya Watanzania wanaotaka kuona wananyakua taji hilo.
Kocha huyo ambaye ni msaidizi wa kocha wa Taifa Stars, Charles Mkwasa, alisema licha ya kushinda michezo miwili ya kundi hilo, hataidharau Ethiopia na atashusha kikosi cha nguvu kwa ajili ya kupata ushindi mwingine.
“Nimetumwa na Watanzania taji la mashindano haya na hata baada ya kufuzu kwa robo sitashusha kikosi cha kuidharau Ethiopia katika mchezo wa mwisho, nahitaji pointi tisa katika tisa.
“Soka si mchezo wa kuridhika, kila kitu kinatakiwa kuonekana kama kimefanyiwa kazi hivyo nahitaji ushindi katika kila mchezo,” alisema Kibadeni.
Wakati huohuo, Wenyeji Ethiopia wamepata ushindi wa kwanza kwa kuifunga Somalia 2-0.
Mabingwa watetezi Kenya ililazimishwa sare 1-1 na Burundi, wakati Malawi ikijihakikishia kucheza robo fainali baada ya kuifunga Djibout katika mchezo wa Kundi C.
SOURCE:Mwananchi
Maoni
Chapisha Maoni