Makinda: Lissu, wenzake acha kabisa!



Anne MakindaAnne Makinda 

Dar/Dodoma. Spika wa Bunge Anne Makinda ametangaza rasmi kutogombea tena nafasi hiyo, huku akisema kulikuwa na wabunge watundu wanane waliomchangamsha na kumlazimisha ajifunze kwa haraka baadhi vifungu vya kanuni za Bunge.
Makinda amekuwa mbunge tangu mwaka 1975 na alikuwa Spika kwa kipindi cha mitano, wakati Samuel Sitta akiwa Spika yeye (Makinda) alikuwa naibu wake.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kwenye ofisi za Bunge jijini Dar es Salaam, alisema atawakumbuka wabunge hao waliomchangamsha kwenye Bunge la 10, kwa kuibua hoja za nguvu.
Aliwataja wabunge hao kuwa ni Halima Mdee, Tundu Lissu, Ezekiah Wenje, John Mnyika wote wa Chadema, Ester Bulaya (wakati huo alikuwa CCM), Felix Mkosamali na Moses Machali wote waliwa NCCR-Mageuzi na Deo Filikunjombe wa CCM (kwa sasa ni marehemu).
“Nitawakumbuka sana rafiki zangu, walikuwa wachangamfu kiasi cha kufanya nizijue kanuni kwa nguvu, mara ya kwanza kuanza kazi nilishituka, lakini baadaye nikajifunza kumbe hivi ndivyo ilivyo, kwa kweli lilikuwa bunge zuri,” alisema.
Alidai kusikitishwa na baadhi ya wabunge kushindwa kwenye majimbo yao akiwamo Wenje katika Jimbo la Nyamagana na kumsihi asikate tamaa badala yake ajipange kwa wakati mwingine.
Makinda alisema fujo za baadhi ya wabunge zililifanya Bunge aliloliongoza kuwa na mvuto wa aina yake, kwa madai kuwa likipoa haliwezi kuleta maana ya kuwapo kwa chombo hicho.
Alikiri kujifunza mambo mengi kwenye Bunge aliloliongoza kutokana na kuwapo kwa wabunge wengine vijana.
“Kuna mabunge ya nchi nyingine ambayo tumeshuhudia watu wakitwangana, Bunge halitakiwi kupoa lazima wawepo watundu wa kulichangamsha, vinginevyo litalala na kukosa mvuto,”alisema Makinda.
Alisema jambo alilojifunza kwenye Bunge hilo, ni kutokuwa na hasira, kuwa mvumilivu, huku akijitahidi kupokea hoja za wabunge wote bila kubagua wala kuwapo upendeleo kwa wabunge wa chama chake (CCM).
Makinda alisema ubunge ni uwakilishi wa wananchi na kwamba, baadhi ya wabunge ambao hawakufanya kazi zao ipasavyo kwenye Bunge lililoisha, walichangia kukwamisha kura za chama chake.
Aliwataka wabunge kuwatumikia wananchi waliowachagua kwenye majimbo yao badala ya kutumia muda mwingi, kutengeneza hoja za uongo bungeni.
Makinda (pichani) ambaye alikuwa mbunge wa jimbo la Njombe Kusini (CCM), alisema amelazimika kustaafu nafasi hiyo ili awaachie wengine waongoze, baada ya kuwapo bungeni kwa miaka 40.
“Maisha yangu yote nimekuwa mwanasiasa, nimeshakuwa kiongozi wa nafasi zote bungeni kwa hivyo nimeamua kustaafu uongozi, nafikiri ni jambo zuri kuachia wengine waendelee kuongoza,” alisema.
Sifa za Spika ajaye
Alisema Spika anayetakiwa ni lazima akubali kujifunza tabia za wabunge wake na kuwa na uwezo wa kukabiliana na hali halisi ya bungeni.
Alisema ni lazima spika huyo awe mvumilivu na asiwe mwepesi wa hasira badala yake atumie muda wake kujifunza kanuni za Bunge na kuwa mwepesi wa kupokea hoja za wabunge bila kubagua ili azifanyie kazi.
“Akubali kuwa rafiki wa wabunge wote ili baada ya Bunge, maisha mengine yaendelee. Nilikuwa rafiki wa wabunge wote na sikuwa mwepesi wa kukasirika,” alisema.
Wabunge watua Dodoma
Wakati Makinda akisema hayo, Mjini Dodoma, baadhi ya wabunge wateule wamesema Spika wa Bunge la 11 anatakiwa kuwa mtu mwenye hekima, uvumilivu na mwenye kuhimili mikiki mikiki ya wabunge ambao wengi wao ni vijana na wapya.
Mbunge wa Buyungu (Chadema), Kasuku Bilago alisema Spika anayetakiwa ni mtu makini na mwenye kuhimili mikiki mikiki ya wabunge hao. “Siyo shughuli ndogo katika Bunge hili. Spika anayekuja anatakiwa kuepuka upande,” alisema Bilago.
Daniel Mtaka wa Manyoni Mashariki- (CCM), alisema: “Spika aendane na wakati. Tunahitaji asiwe mtu wa kukariri, achukue mawazo mazuri ya kujenga nchi hata kama yanatoka kwenye upinzani.”
Mbunge wa Konde (CUF), Khatibu Said Haji alisema Spika anayetakiwa ni yule atakayetoa uhuru wa wabunge kuisimamia Serikali na kutozima hoja za wabunge.
Vita ya Uspika
Kampeni za uspika zilikuwa zikiendelea jana katika Viwanja vya Bunge, huku baadhi ya wabunge wateule wanaomuunga mkono Naibu Spika wa Bunge la 10, Job Ndugai wakitafuta kura kutoka kwa wabunge wenzao wa CCM.
Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde alisema kampeni za kumpata spika na naibu wake ndani ya CCM zimeshamalizika, kutokana na wabunge wengi kumuunga mkono Ndugai ambaye ni mbunge mteule wa Kongwa, .
Kwa upande wa naibu spika wanayemtaka ni Mbunge mteule wa Ilala, Azan Zungu ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bunge katika Bunge la 10.
Zungu jana alikuwa mwanachama wa kwanza wa CCM kuchukua fomu akiwania nafasi ya naibu spika, tofauti na matarajio ya wengi kuwa angewania uspika.
Alisema asingetaka uspika kwa sasa, kwani bado anaendelea kujifunza uongozi wa chombo hicho na sehemu sahihi kwa sasa ni nafasi ya unaibu spika.
Mbunge mteule wa Kasulu Mjini, Daniel Nsanzugwanko, jana alikuwa kada wa CCM wa 23 kuchukua fomu kuwania uspika.
Akizungumza wakati wa kurudisha fomu Nsanzugwanko alisema amejitokeza kuwania nafasi hiyo kuliwezesha Bunge kuisaidia Serikali ya awamu ya tano iweze kukidhi kiu ya Watanzania.
Mbali na usajili wa Bunge, maofisa kutoka benki za CRDB na NMB walikuwa wakitoa huduma kwenye viwanja hivyo zikiwamo za mikopo katika mahema kadhaa yaliyofungwa hapo.
Kwa upande wa mavazi, wabunge wengi walionekana kutomudu mavazi yanayohitajika katika kupiga picha.
“Mimi imenibidi kurudi nyumbani kuvaa koti maana wamesema siwezi kupiga picha bila kuvaa koti,” alisema mmoja wa wabunge kutoka kanda ya kusini. Mavazi mafupi yalionekana kutawala kwa wabunge wengi wa kike vijana katika viwanja hivyo.










SOURCE:Mwananchi


























































































Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

USAJILI WENYE MANUFAA EPL HADI SASA..