Samatta kulamba Sh1.6 bilioni Ulaya...



Mbwana SamattaMbwana Samatta 
Dar es Salaam. Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania na klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Mbwana Samatta yuko mbioni kujiunga na klabu ya Ligi Kuu Ufaransa (Ligue 1), Lllle kwa Euro 700,000, sawa na (Sh1,611,675,675.99 za Tanzania.
Kwa mujibu wa mtandao wa francefootball.fr, mshambuliaji huyo anayewania tuzo ya mwanamichezo bora wa mwaka wa Afrika kwa wachezaji wa ndani atajiunga na miamba hiyo ya Ufaransa wakati wa usajili wa dirisha dogo Ulaya mwezi Januari.
Rais na mmiliki wa klabu yake ya TP Mazembe, Moise Katumbi alisema baada ya timu yake kuchukua ubingwa wa Afrika wameshafikia makubaliano na klabu ya Lille kuhusu azma ya kumuuza nyota huyo.
Katumbi amelithibitisha hilo alipozungumza na kituo cha redio cha RFI kupitia kipindi chake cha International Foot na kuwa Samatta atajiunga na Lille inayonolewa na kocha wa zamani wa Zambia, Herve Renard baada ya kumalizika kwa mashindano ya Klabu Bingwa ya Dunia yatakayofanyika Japan kuanzia Desemba 10 hadi 20.
“Klabu nyingi za Ulaya zimekuwa zikimhitaji Samatta, lakini makubaliano yetu yameenda vizuri na klabu hiyo ya Ufaransa inayonolewa na Renard. Ninakujulisha kwamba uhamisho wa Samatta kwenda Lille utafanyika baada ya mashindano ya Dunia ya Klabu mwezi ujao,” alinukuliwa Katumbi.
Mapema Februari mwaka huu, Samatta alitakiwa na klabu ya Standard Liege ya Ubelgiji, lakini Katumbi alikataa kumuuza mshambuliaji huyo.
Baadaye, alifanya majaribio kwenye timu ya CSKA Moscow ya Russia, lakini alipata majeraha yaliyomlazimu kukatisha majaribio hayo.
Msimu huu unaomalizika amekuwa wa mafanikio baada ya kuiongoza TP Mazembe kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika wiki iliyopita, akifunga mabao saba ambayo yamemfanya awe mfungaji bora, huku pia akiingia kwenye orodha ya wachezaji 10 wanaowania tuzo ya mwanasoka bora kwa wachezaji wa ndani barani Afrika.
Samatta alijiunga na TP Mazembe akitokea Simba kwa gharama ya uhamisho wa Sh150 milioni mwaka 2011, tangu wakati huo amekuwa na mchango mkubwa kwa mabingwa hao wa Afrika.

Siri ya mafanikio ya Samatta yafichuka
Nidhamu aliyonayo Samatta katika soka inatokana na kazi ya upolisi waliyokuwa wakiifanya wazazi wake.
Akitoboa siri hiyo, baba mzazi wa Samatta, Ally Pazi Samatta, alisema, “Mimi na mama yake tulikuwa makamanda wa polisi. Kazi ambayo kwa kipindi hicho ilihitaji nidhamu ya hali juu ndiyo maana hata vijana wetu wakalelewa hivyo,” alisema.
“Pamoja na hilo pia mimi nilikuwa mchezaji wa Simba na Taifa Stars, hilo pia lilitosha kuwaongoza vijana wangu kujua nidhamu ya soka ili waweze kufika mbali, nashukuru Mungu, limetimia kwa Mbwana ingawa wengine wameishia kucheza Ligi Kuu Bara,” alisema.
Baba mzazi wa staa huyo alisema kuwa kati ya mambo anayomsisitiza mwanaye ni nidhamu ikiwa pamoja na kumtanguliza Mwenyezi Mungu kwa kila jambo.
“Samatta na kaka yake, Mohemed Samatta anayecheza JKT Mgambo, nimewawekea faini pale wanapoonyesha kukosa nidhamu uwanjani, kwa hiyo wamekuwa wakizingatia sana maelekezo hayo,” alisema.
Aliongeza, “Siku moja nilipowaambia mtu akikosa penalti anatakiwa kulipa Sh2,000, walicheka, lakini nilipofafanua kuwa watalazimika kuleta nyumbani moja kwa moja bila kutuma sehemu yoyote hata kama Samatta atakuwa Mazembe itambidi asafiri kuja ndipo walipoona ugumu wa adhabu, hiyo lengo ni kuona wanakuwa makini kila eneo.”







SOURCE:Mwananchi














































































Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

USAJILI WENYE MANUFAA EPL HADI SASA..