Chadema Mbeya walalamikia uteuzi wabunge viti maalumu...


Mbeya. Uteuzi wa wabunge wa viti maalumu kupitia Chadema umezua taharuki mkoani hapa na Kanda ya Nyanda za Juu kwa ujumla baada ya wanachama na viongozi wa chama hicho kuanza kulalamikia wakidai umetumika upendeleo.
Walalamikaji wanasema  wanachama wa kike ambao  walikuwa mstari wa mbele kukisaidia chama ‘wametemwa’ na kuteuliwa wanawake ambao  kimsingi hawakuonyesha ushiriki kikamilifu katika chama na wa wananchi wa eneo husika.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya wagombea Ubunge kupitia Chadema na Ukawa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Jacob Kalua alisema kuna ubabaishaji na upendeleo usiokuwa na tija katika uteuzi wa wabunge wa viti maalumu uliofanyika ndani ya Chadema kwa vile  walioteuliwa wengine hawajawahi kuonekana majimboni lakini wanashangaaa kuona wamepewa nafasi hiyo.
“Hapa simung’unyi maneno kabisa. Kwa mfano aliyeteuliwa mkoani Ruvuma, hata viongozimkoa huo hawamjui. Kutoka Iringa wameteuliwa watatu, lakini mmoja amejiunga Chadema hivi karibuni na jina lake linateuliwa. Hapa Mbeya ameteuliwa mmoja, lakini ushiriki wake kwenye chama unazidiwa na wanawake wengine walioomba nafasi hiyo waliopo hapa na huko mkoani Songwe ambako kuna majimbo matatu  ya Chadema hajateuliwa mwanamke hata mmoja,’’ je hii ni halali?, alihoji.
Naye Katibu wa Chadema, Wilaya ya Mbarali Nicolaus Lyaumi alisema anashangazwa  kuona majina ya wabunge walioteuliwa siyo wale waliotarajiwa  na wanachama wengi mkoani Mbeya.
“Unajua lengo la wabunge hawa ni kusaidia ujenzi wa chama mkoa na wilaya husika , lakini sasa kwa uteuzi huu tunaamini kabisa bado kuna sintofahamu iliyo mbele yetu kwani watu waliomba wamepigwa chini,” alisema.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Joseph Mwachembe maarufu kwa jina la ‘China’ alipoulizwa kuhusu suala hilo, alisema hawezi kuzungumzia chochote akisema hajapata orodha kutoka kwa viongozi wake na kwamba majina yaliyotangazwa hayaamini.
Alisema ‘binafsi kama mkoa bado hatujaletewa rasmi majina ya wateule. Hivyo tukiletewa tutakaa na viongozi wenzangu mkoa tutayachambua na ndipo nitakuwa na la kusema itakapobidi’.








SOURCE:Mwananchi






























































































































Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

USAJILI WENYE MANUFAA EPL HADI SASA..