Haya ndiyo matamanio ya Watanzania kwa Dk Magufuli..

Rais Mteule wa Serikali ya Awamu ya Tano, DkRais Mteule wa Serikali ya Awamu ya Tano, Dk John Magufuli.
Dar/Mikoani. Siku moja baada ya Rais Mteule wa Serikali ya Awamu ya Tano, Dk John Magufuli kukabidhiwa cheti chake kuwa ndiye mshindi katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, wananchi wakiwamo wa kada mbalimbali wameelezea hisia zao na matanio yao kuona atatekeleza ahadi alizotoa kwenye mikutano yake ya kampeni.
Dk Magufuli (CCM) alitangazwa mshindi wa urais na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) katika uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 25 kwa kupata kura 8,882,935 huku mpinzani wake, Edward Lowassa (Chadema) akiambulia 6,728,480. Wagombea wanane walikuwa wakiwania kiti hicho kupitia vyama vingine vya siasa.
Wasomi
Mhadhiri wa Chuo cha Saut Tawi la Mtwara, Michael Okoda alisema anafurahi kwa kuwa uchaguzi huo ulifanyika kwa amani na utulivu na kwamba Dk Magufuli anatakiwa kutekeleza ahadi alizotoa kwa wananchi wakati akijinadi kwao kwenye mikutano ya kampeni.
Alizitaja baadhi ya ahadi hiyo kuwa ni elimu bure, afya na ajira kwa kuwa walioshiriki kumpigia.
Mwenyekiti wa Umoja wa Jumuiya ya Vyuo Vikuu na Vyuo Vishiriki (Asas), Paul Losolutie, alisema anataka kuona mahakama ya wezi na mafisadi inaundwa nchini na Tanzania inakuwa nchi ya viwanda kama alivyoahidi Magufuli kwenye kampeni.
Azaki
Mratibu wa Taifa wa Taasisi ya Wanawake ya Ulingo, Dk Ave Maria Semakafu, alisema anaamini wanawake wengi wamefurahishwa na ushindi huo kwa sababu kwa umewezesha pia kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi kuwa na Makamu wa Rais mwanamke, Samia Suluhu Hassan.
“ Tumefungua ukurasa mpya kwani miaka 20 ya tamko la Mkutano wa wanawake Duniani wa mwaka 1995 Beijing, tumekuwa na mrejesho mzuri kuhusu mwitikio wa Serikali kuweka ushiriki sawa wa nafasi za uongozi,” anasema Dk Semakafu .
Beatrice Jesta wa RRM, alisema wanachosubiri kwa sasa ni Dk Magufuli kuanza kuwasafisha wezi wa fedha za umma na kuijenga nchi katika mazingira ya umoja na mshikamano.
Mwenyekiti wa Kamati ya Amani mkoa wa Arusha (APET), Petro Ahham anasema uchaguzi umemalizika kwa amani katika maeneo mengi jambo ambalo ni la kujivunia kwa Watanzania.
“Nchi nyingine leo kungekuwa hakuna amani, lakini uchaguzi umekwisha kwa amani na sisi hapa Arusha amani imekuwa nzuri zaidi tunapongeza wadau wote kwa kufanikisha amani, ’’ anasema.
Wachambuzi
Prince Mwaihojo, mchambuzi wa masuala ya siasa mkoani Mbeya anasema ushindi wa Dk Magufuli umeinusuru nchi kuporwa na waroho wa madaraka.
Alisema Tanzania ya sasa inamhitaji kiongozi kama Magufuli ambaye alitangaza kwamba atawatumikia Watanzania wote na kuwaunganisha kuwa na umoja bila kujali itikadi za vyama vya siasa.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Chaumma, Kayumbu Kabutale anasema kama Dk Magufuli hataweza kufanya mapinduzi katika mfumo wa CCM na kutekeleza ahadi alizotoa kwa wananchi wakati wa kampeni na kubaki kuwa ndoto.
Wananchi
Yusuph Mwikoki, mkazi wa Songea, amemtaka Dk Magufuli atimize ahadi alizotoa na asifanye kazi kwa mazoea kwa kuwa Watanzania wana matarajio makubwa katika uongozi wake.
Akitoa maoni yake, mkazi wa mtaa wa Mwambene wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Edson Chuma alisema ushindi wa Dk Magufuli ni kauli ya Watanzania wasiotaka kupelekeshwa kama ng’ombe.
Hamis Abdallah Ally, mkazi wa Maposeni Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma alisema anasubiri kuona Dk Magufuli akiwakamata na kudhibiti mafisadi na kurejesha imani kwa wananchi.
Kelvin Chale wa Manispaa ya Songea, alimtaka Dk Magufuli kuboresha mazuri ya Rais Jakaya Kikwete na kushugulikia kero za wananchi.
Neema Komu, mkazi wa Kibaha, Pwani alisema hana mpango wa kuandaa ada wala michango ya shule kwa watoto wake kwani anaamini mgombea aliyepita atafuta yote kama alivyoahid kwenye kampeni.
“Kwa sasa ninaandaa sare tu kwa mwanangu anayetarajia kuanza masomo mwakani kwani hatutakuwa na masuala ya ada,” alisema
Irine Nkya alisema : “Tunamtarajia Dk Magufuli afanye kazi kwa bidii, juhudi na maarifa huku akiwachukulia hatua kali watumishi wazembe kama alivyowaahidi Watanzania.”
Paul Shija, mkazi wa Urambo mkoani Tabora, alisema Rais Magufuli atekeleze ahadi kwa wananchi kwa kutatua kero zao kwa sababu ameonyesha ana uwezo wa kuwatumikia.
Mkazi wa mkoani Geita, Shaaban Jumanne alisema ana matarajio makubwa na Magufuli kwa kuwa wakazi wenzake uchumi wao mkubwa ni uchimbaji wa madini na hivyo atimize ahadi yake.
Masanja Maduhu alisema: “Dk Magufuli alivyopita kwao kuomba kura aliahidi kuwapa maeneo ya uchimbaji wananchi, sasa tunamuomba atimize ahadi yake.”
Mery Ndoshi wa Geita, alisema mji wao unakabiliwa na kero sugu ya kukosa maji safi na salama ambayo Magufuli wakati wa kampeni aliwaahidi kuitatua na kujenga vyumba vya madarasa.
Falesi Bunini, mkazi wa Kata ya Kwanga mkoani Mara, alisema angependa kuona Dk Magufuli akitekeleza ahadi ya kuwalipa wazee fedha za kujikimu kwa maisha na matibabu bure.
Joseph Haule mkazi wa kata ya Rwamlimi alikumbusha ahadi ya kukuza uchumi na kuhakikisha thamani ya shilingi inaongezeka ili kukabiliana na mfumo wa bei na maisha ya Watanzania kuzidi kuwa magumu.
Mkazi wa Pansiasi mkoani Mwanza, Celine Paul alisema tatizo la ajira kwa vijana ni kati ya mambo aliyoahidi kutatua..
Peter Mwita, mkazi wa Igoma, Mwanza alisema anatarajia Magufuli ataondoa migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima.
Juma Cosmas, mkazi wa kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga alisema anatarajia kuona viwanda vikifufuliwa, kuanzisha vipya na kuondolewa kwa tatizo la ajira.
Mkazi wa kata ya Kambarage Shinyanga, Amina Yusuph alisema anachotaka kuona ni kuboresha huduma za afya katika miji yote pamoja na upatikanaji wa dawa.
Naye Brayan Mshana alisema kama mwananchi asiyefungamana na upande wowote anakubaliana na matokeo na kikubwa Dk Magufuli atekeleze ahadi alizozitoa kwa wananchi.







SOURCE:Mwananchi








































Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

USAJILI WENYE MANUFAA EPL HADI SASA..