Hospitali ya Bugando imezindua mpango mkakati wa kuboresha huduma za afya.
Hospitali ya rufaa Bugando iliyopo jijini Mwanza imezindua mpango mkakati wa miaka kumi unaolenga kutatua changamoto halisi zilizopo katika hospitali hiyo ili kuboresha huduma bora za afya na zitakazokuwa zinatolewa kwa weledi na kwa wakati kwa kuzingatia maadili ya kazi, huruma na upendo kwa wagonjwa.
Uzinduzi wa mpango mkakati wa hospitali wa miaka kumi (2015 hadi 2025), umefanywa na mwenyekiti wa bodi ya hospitali hiyo, ambaye pia ni askofu mkuu wa jimbo kuu la Mwanza mhashamu baba askofu Jude Thaddaeus Ruwaichi, ambapo amewataka wafanyakazi na viongozi wa hospitali hiyo kutekeleza kwa dhati na weledi wa hali ya juu malengo makuu sita yaliyomo katika mpango huo ili kujenga matumaini mapya kwa jamii ya watu wa kanda ya ziwa.
Mapema, mkurugenzi mkuu wa hospitali ya rufaa Bugando Prof. Kien Mteta amesema mpango mkakati huo unajumuisha malengo sita ya kimkakati ambayo yamejikita katika kuboresha na kuimarisha zaidi huduma za afya za ubingwa mbalimbali katika hospitali hiyo na kuhakikisha zinatolewa kwa usahihi na watumishi wenye weledi na uadilifu wa kiwango cha juu.
Hospitali ya rufaa Bugando inayohudumia mikoa sita ya kanda ya ziwa, ilifunguliwa rasmi tarehe 5 Desemba 1971 na rais wa kwanza wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Hospitali hiyo ilijengwa kwa ukarimu wa watu wa Ujerumani magharibi na Uholanzi kupitia shirika katoliki la Misereor. Serikali iliwahi kuitaifisha hospitali hiyo lakini mwaka 1985 iliirejesha tena kwenye umiliki wa kanisa.
Hospitali hiyo imekuwa ikiendeshwa bila kuwa na mpango mkakati wowote, hii ni kufuatia mpango uliokuwepo huko nyuma kumalizika tangu mwaka 2008 na baada ya hapo hospitali hiyo imekuwa ikiendeshwa kwa kuzingatia mpango wa mwaka mmoja unaoandaliwa kila mwaka.
SOURCE:ITV
Maoni
Chapisha Maoni