NEC: Wanaharakati mpeni utulivu Rais...
Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva amewataka wanaharakati wampe utulivu Rais John Magufuli kuhusu uteuzi wa baraza la mawaziri.
Kauli hiyo ya Lubuva imekuja siku moja baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi kutoa wito kwa Rais Magufuli kuzingatia usawa wa jinsia katika uteuzi wa baraza hilo.
Akizungumza jana, Jaji Lubuva alisema taratibu bado hazijakamilika kumwezesha Rais kutekeleza jukumu hilo. Alisema taratibu zinazomuongoza Rais kutekeleza wajibu wake zipo wazi na kila anachokifanya kuna wasaidizi na washauri anaoshirikiana nao kwa mujibu wa Katiba ya nchi.
“Nimesoma gazeti na kuona TGNP wakimshauri Rais Magufuli kuzingatia usawa wa kijinsia kwenye baraza lake la mawaziri. Hiyo naona haikuwa sawa...Rais atafanya hivyo baada ya mamlaka nyinginezo kukamilisha taratibu zao,” alisema.
Juzi, Liundi alisema lengo la kutaka baraza hilo lizingatie usawa wa jinsia ni kutimiza mkataba uliosainiwa na mtangulizi wake kutekeleza azimio la kimataifa.
Maoni
Chapisha Maoni