Mgombea ubunge adaiwa kumshambulia ofisa wa chama chake...
Marcossy anadaiwa kumshambulia Dimoso katika ofisi za chama hicho zilizopo Mtaa wa Ngoto.
Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Leonald Paulo alisema jana kuwa, Marcossy anadaiwa kufanya tukio hilo mwishoni mwa wiki iliyopita.
Paulo alisema mtuhumiwa huyo alifanya tukio hilo baada ya kumkuta katibu mwenezi huyo kwenye ofisi za chama hicho na baadaye kuondoka.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo ambao hawakutaka majina yao yaandikwe gazetini, walisema mgombea huyo alipofika katika ofisi hizo alianza kumshambulia katibu huyo kwa maneno kuwa anamtangazia kwa wananchi amekula fedha za mawakala waliosimamia kura zake wakati wa uchaguzi.
Walisema mbali ya kumshambulia kwa maneno, pia alimpiga wakiwa ndani ya ofisi hiyo. Mashuhuda huo walisema wakati tukio hilo linatokea katika ofisi hizo, ndani walikuwamo baadhi ya viongozi wa chama hicho ambao waliuamua ugomvi huo na kisha kumuondoa mgombea huyo katika eneo hilo.
Alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo, Dimoso alikiri kushambuliwa kwa kupigwa na mgombea huyo akimtuhumu kwa mambo mbalimbali, ikiwamo madai ya kumtangazia kuwa amekula fedha za mawakala, suala ambalo siyo kweli.
Alisema kutokana na shambulio hilo pamoja na kupewa vitisho alilazimika kwenda kufungua kesi katika Kituo Kikuu cha Polisi Morogoro, huku suala hilo likishugulikiwa na viongozi wa juu wa Chadema.
Akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hii, Marcossy alisema kwa sasa hawezi kusema lolote kwa kuwa hajapata taarifa zozote kutoka Jeshi la Polisi.
“Mimi nipo na hakuna barua yoyote wala taarifa kutoka Jeshi la Polisi niliyopata kama natafutwa, hivyo nasubiri hilo na nitawajuza,” alisema.
Kuhusu mawakala waliokuwa wanasimamia matokeo yake kwenye Uchaguzi Mkuu inaodaiwa hawajalipwa, alisema hajui lolote na kuwataka wawaulize waliowatafuta kuliko kumtupia lawama yeye. Alisema mawakala hao walipotafutwa walipewa maelezo nani atayehusika kuwalipa fedha zao, hivyo anawashangaa kuambiwa kwamba amekimbia na fedha zao.
Katibu wa Chadema mkoa wa Morogoro, Samuel Kitwika alipoulizwa juu ya taarifa ya kushambuliwa kwa katibu mwenezi na mgombea huyo, alisema hajui lolote na kwamba hajapokea malalamiko mpaka sasa.
Kitwika alisema chama hicho kipo shwari na kama atafikishiwa malalamiko, hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya mhusika.
Alisema kwamba, zipo taratibu za kushughulikia malalamiko yanayofikishwa kwa uongozi. Katibu huyo alisema milango ipo wazi kwa kuwa chama hicho ni taasisi yenye utaratibu wa utendaji.
Maoni
Chapisha Maoni