Jibu la Waziri Mkuu...
Rais John Magufuli
Dodoma/Dar/Mikoani. Wakati jina la Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tano litajulikana leo baada ya Rais John Magufuli kuliwasilisha bungeni, wananchi wametoa maoni tofauti kuhusu mtu anayetakiwa kupewa nafasi hiyo ya mtendaji mkuu wa Serikali.
Kwa mujibu wa Katiba, Rais anatakiwa awasilishe pendekezo la jina la Waziri Mkuu bungeni kwa kumpa Spika ambaye anatakiwa awatangazie wabunge na baadaye kumpigia kura.
Ili athibitishwe na Bunge, mtu aliyependekezwa kuwa Waziri Mkuu ni lazima awe mbunge wa kuchaguliwa jimboni na anatakiwa apitishwe na theluthi mbili ya wabunge.
Kuidhinishwa kwa Waziri Mkuu kutampa mwanya Rais kuanza kutengeneza “Serikali ya Magufuli” kwa kushirikiana na mtendaji huyo mkuu wa Serikali. Mtu wa kwanza kuteuliwa na Rais alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju.
Tayari Tanzania imeshakuwa na watu kumi walioshika nafasi hiyo, wakiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere, aliyekuwa Waziri Mkuu mara baada ya nchi kupata uhuru.
Alifuatiwa na Rashid Kawawa, Edward Sokoine, Joseph Warioba, Cleopa Msuya, John Malecela, Salim Ahmed Salim, Frederick Sumaye, Edward Lowassa na Mizengo Pinda. Lowassa na Pinda wameshika nafasi hiyo katika kipindi cha miaka 10 ya Serikali ya Awamu ya Nne.
Kumekuwapo na ubashiri mkubwa wa jina la mtu atakayeshika wadhifa huo, wengi wakibashiri kutokana na utamaduni ambao chama tawala, CCM, kimekuwa kikiutumia katika kipindi cha uongozi wake.
Wapo wabunge ambao wamekuwa wakitajwa kutokana na kanda wanazotoka, utendaji wao, uadilifu na uzoefu wao serikalini, lakini bado suala hilo limekuwa siri kubwa ya mkuu wa nchi na wanaomzunguka.
Kati ya wabunge ambao wametajwa sana ni pamoja na William Lukuvi, mbunge wa Isimani mkoani Iringa, ambaye amejihusisha na chama hicho kuanzia ngazi ya vijana hadi sasa na pia ana uzoefu serikalini baada ya kutumikia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kipindi kirefu akiwa waziri wa kawaida.
Pia yumo January Makamba (Bumbuli), ambaye anajulikana kwa utendaji, Kassim Majaliwa(Ruangwa), ambaye pia alikuwa Naibu Waziri wa Tamisemi, Dk Harrison Mwakyembe (Kyela), aliyeongoza wizara za Usafirishaji na Uhusiano wa Afrika Mashariki na Ramo Makani (Tunduru Kaskazini).
Tofauti na nyakati nyingine ambazo habari za mbunge aliyeteuliwa na Rais huanza kusikika kutokana na kuonekana ameongezewa ulinzi, hali ni tofauti mwaka huu kwa kuwa mabadiliko hayaonekani kwa wabunge wanaotajwa.
Wabunge wengi walionekana kwenye viwanja vya Bunge wakijishughulisha zaidi na kazi ya uapishwaji iliyomalizika jana, baadhi yao wakichukua picha za ukumbusho pamoja na ndugu na jamaa waliofika mjini hapa kuwasindikiza kwenye tukio hilo la kihistoria.
Wakati hayo yakiendelea, John Malecela, ambaye alikuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, amesema mtu anayetakiwa kushika wadhifa wa mtendaji mkuu wa Serikali anatakiwa kuwa na sifa tatu.
“Kwanza, mnyenyekevu, pili awe muadilifu na mpenda watu,” alisema Malecela akiwa nyumbani kwake wakati akipokea vifaa vya kimila kutoka kabila la Wasonjo.
Alisema sifa hizo zitasaidia katika vita aliyoitangaza Hayati Baba wa Taifa, Julius Nyerere katika mapambano dhidi ya umasikini, ujinga na maradhi.
Sifa nyingine ambayo aliitaja ni kuwa na “fimbo ya umoja” baina yake na wabunge wa Bunge la Muungano ili awe kiungo kati ya wabunge na Rais.
Mkongwe huyo katika siasa aliwasifu wabunge wa bunge la Muungano kwa kumchagua Job Ndugai kuwa Spika, akisema ana imani kubwa na kiongozi huyo kwani anaweza kuwasaidia wabunge na taifa kwa ujumla.
Maoni ya wananchi
Wakati nchi ikisubiri jina la Waziri Mkuu, wananchi waliohojiwa na gazeti hili walisema wangependa kiongozi huyo wa shughuli za Serikali bungeni awe mwadilifu, asiyejikweza, asiye na ubaguzi na mnyenyekevu.
“Awe mtu wa kujishusha anayeweza kuzungumza na watu wa aina zote, lakini pia akiangalia maslahi mapana ya nchi,” alisema Marko Kishola,mkazi wa Geita. Aliongeza kuwa Waziri Mkuu anatakiwa awe mtu anayeweza kusimamia mawazo yake na kusimamia haki kwa wote.
Lakini Evarist Stephen, mkazi wa Ndembezi, Shinyanga alikuwa na mawazo ya ziada.
“Nafasi ya Waziri Mkuu inahitaji mtu ambaye atakuwa ni mchapakazi kwa kuwa ndiye mtendaji mkuu wa shughuli za serikali,” alisema Stephen.
“Akiwa legelege hakuna mabadiliko yoyote yatakayopatikana. Lakini pia, ili kumpa nguvu ya utendaji na uwajibikaji, ni vizuri mfumo uliopo wa Katiba ukabadilishwa na Waziri Mkuu apewe mamlaka ya kuwawajibisha watendaji wote walioko chini yake, mfano mawaziri, makatibu wakuu na wakuu wa mikoa badala ya kusubiri uamuzi wa Rais.
Sifa ya utendaji pia ilizungumzwa na mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Hamad Salim aliyesema sifa ya kwanza anayotarajia kwa Waziri Mkuu atakayetangazwa leo ni utendaji mzuri.
“Hiyo haipingiki, lazima awe mtu mtendaji mwenye uwezo wa kusimamia na kutekeleza shughuli za Serikali bila kusahau kulinda Katiba ya nchi,” alisema.“Mtu mwenye utaifa zaidi kuliko uchama.”
Alitaja sifa nyingine kuwa ni uadilifu, hekima , busara, mbunifu na atakayeweza kupambana na ufisadi.
Maoni
Chapisha Maoni