Wazanzibari walichovya vidole mara mbili..

Maalim Seif Sharif Hamad akiinua juu mkono wakeMaalim Seif Sharif Hamad akiinua juu mkono wake baada ya kupakwa wino kuonyesha tayari amepig 

Dar es Salaam. Wakati wapigakura wa Tanzania Bara walitakiwa kuchovya kidole mara moja kuthibitisha kuwa wametumia haki yao ya kidemokrasia kuchagua viongozi wa kitaifa, Tanzania visiwani ilikuwa tofauti; walichovya vidole mara mbili.
Hii inamaanisha kuwa Wazanzibari walipiga kura mara mbili tofauti na wenzao wa Bara.
Kwa hiyo, Wazanzibari walitakiwa kwanza kupiga kura kwa ajili ya kumchagua Rais wa visiwa hivyo viwili vikubwa, wawakilishi wao na madiwani, na pili Rais wa Jamhuri ya Muungano na wabunge.
Nikiwa mmoja wa waandishi wa habari waliopangwa kisiwa cha Pemba kuripoti habari za Uchaguzi Mkuu, nilitembelea vituo kadhaa kushuhudia kazi hiyo na kuona tofauti hiyo ya upigaji kura kati ya Bara na Visiwani.
Mwananchi wa Zanzibar alipofika kituoni, alitakiwa kupanga mstari kama ilivyo Bara na baada ya kufika mbele alionyesha kitambulisho chake kwa mtumishi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
Baada ya karani huyo kuona jina la mwananchi huyo, alilitangaza kwa sauti ili wasimamizi wasikie na kuridhia, kama ambavyo inafanyika Bara.
Baada ya hapo, mtendaji mwingine aliingiza namba za kitambulisho hicho kwenye vishina vya karatasi za kupigia kura na baadaye kuzigonga muhuri kabla ya kumkabidhi mwananchi karatasi hizo ili apige kura.
Hatua hiyo ilifuatiwa na mpigakura kuweka alama ya kura yake kwenye karatasi hizo katika kibanda cha kupiga kura na baadaye kwenda kutumbukiza kwenye maboksi ya kura za wanaowania uongozi Zanzibar, yaani maboksi ya ZEC.
Baada ya kumaliza kazi hiyo, mpiga kura huyo alitakiwa kuchovya kidole kwenye wino na kwenda meza ya pili kwa ajili ya kuhakikiwa na watumishi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Baada ya kuhakikiwa, walipiga kura na baadaye kuchovya kidole cha pili kuthibitisha ameshapiga kura.
Lakini kuna wapiga kura ambao walipiga kura mara moja tu.
“Hawa ni Watanzania waliopoteza sifa za kupata kitambulisho cha Mzanzibari Mkazi kutokana na kutoishi Zanzibar mfululizo kwa miaka mitano,” alisema Ali Mohamed Dadi, ofisa mdhamini wa ZEC, ofisi ndogo ya Pemba.
Watanzania hao walienda moja kwa moja kwenye daftari la NEC na kuhakikiwa kabla ya kupewa karatasi za kupigia kura. Baadaye walichovya kidole na kuondoka.
Kwa ujumla niliona idadi kubwa ya wanawake wakishindwa kupiga kura kutokana na mchakato huo kuwa mrefu.
“Asilimia 85 ya wanawake walisaidiwa kupiga kura kwa sababu karatasi za kupigia kura kuwa nyingi wakati hawakuwa na elimu ya kutosha ya mpigakura,” alisema Bakari Rajab, msimamizi wa kituo cha Skuli ya Ng’ombeni, Pemba.









SOURCE:Mwananchi











































































































Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

USAJILI WENYE MANUFAA EPL HADI SASA..