Katibu Mkuu aisikitikia NCCR, asema historia itawahukumu...
Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe.
Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Nyambabe alisema hana jipya la kuzungumza kwa sababu alishazungumza kuhusu mustakabali wa chama chao ndani ya Ukawa, huku akisisitiza namna ambavyo historia itawahukumu.
“Sina la kusema kwa sasa, nilizungumza sana kuhusu kinachoendelea ndani ya Ukawa. Nilisema historia itatuhukumu, niliona mbali, niliyoyazungumza hayajapitwa na wakati,” alisema.
Novemba, mwaka huu viongozi wa chama hicho akiwamo Makamu Mwenyekiti (Bara), Leticia Mosore, katibu mkuu, baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na viongozi wengine walizungumza na waandishi wa habari na kuonyesha shaka ya chama chao kuwa ndani ya Ukawa.
Katika mkutano huo uliofanyika Hoteli ya Landmark, Dar es Salaam, viongozi hao walitoa tamko kwa kile walichodhani ni anguko la chama chao kuwa ndani ya Umoja huo wa Katiba ya Wananchi.
Akitoa tamko hilo, Mosore alisema kuwa miongoni mwa mambo waliyokubaliana katika umoja huo ni namna ya kujiendesha, ikiwamo kuunda kamati za kutatua matatizo kama Kamati ya Makatibu Wakuu, Kamati ya Ufundi na Kamati ya Wataalamu walizodai zimeshindwa kufanya kazi ipasavyo.
Alisema viongozi hao wameshindwa kuweka kanuni za uendeshaji na kuacha mambo yafanyike kiholela, kamati kushindwa kushughulikia migogoro baina ya vyama, kushindwa kuunda na kusimamia kamati za majimbo na kushindwa kufikia muafaka wa kuachiana majimbo.
Tamko hilo lililenga zaidi kulalamikia ufinyu wa majimbo 12 waliyopewa ikilinganishwa na majimbo 67 waliyosimamisha wagombea mwaka 2010 wakiwa wa kama chama kinachojitegemea.
Mosore pia alilalamikia kuwa licha ya chama chao kurudishwa nyuma, wanahujumiwa kwa sababu bado wanachama wa vyama vingine vilivyo ndani ya umoja huo walikuwa wanang’ang’ania kusimamisha wagombea kwenye baadhi ya majimbo ya uchaguzi.
Akizungumza katika mkutano huo ulionyimwa baraka na chama ngazi ya Taifa, Nyambabe alizitaja kasoro nyingine kuwa ni kushindwa kukubaliana katika baadhi ya mambo aliyodai mwenyekiti wao amekuwa akiyafumbia macho, ikiwamo kushindwa kupata muafaka wa namna ya kuachiana wagombea udiwani.
Suala jingine alilolalamikia ni kushindwa kuonyesha na kukubaliana kila chama kitapata nafasi gani na ngapi iwapo Ukawa ungeshinda na kuunda Serikali, kushindwa kufuata utaratibu wa kumpata mgombea urais wa umoja huo na kuwapa umuhimu mkubwa wanachama kutoka CCM.
Nyambabe pia alilalamikia kutokuwa na timu ya kampeni ya umoja huo ambayo ingewasaidia wagombea wote na Chadema kuwa na nguvu kubwa katika umoja huo ikiwamo kutumia fedha inavyotaka.
Viongozi hao pia walitoa wito wa kumshauri Mwenyekiti wao, James Mbatia aitishe vikao vya kikatiba ili wajadiliane kuhusu hatima ya chama chao.
Mjumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho na aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Kigoma Kusini, David Kafulila ambaye ameshindwa aliliambia gazeti hili kuwa hana la kusema juu ya madai hayo kwa sababu siyo msemaji wa chama hicho.
Alisema chama hicho kitakuwa na mkutano na waandishi saa tano asubuhi leo na majibu yote ya mustakabali wa chama yatatolewa.
Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia alipopigiwa simu zote mbili zilikuwa zinaitwa bila majibu.
Katika uchaguzi uliofanyika Jumapili iliyopita, chama hicho kilipata jimbo moja tu la ubunge la Vunjo ambalo ameshinda Mbatia. Kabla ya uchaguzi huo kilikuwa na majimbo manne ya Kigoma Kusini, Kasulu Mjini, Kasulu Vijijini na Muhambwe, lakini katika uchaguzi majimbo hayo yamepotea.
Maoni
Chapisha Maoni