Spidi ya Dk Magufuli inajibu maswali yaliyokosa majibu...



Rais wa Awamu ya Tano, Dk John MagufuliRais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli.
Kabla hajaapishwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli alitamka kuwa mara atakapoapishwa ataanza kazi mara moja.
Alitekeleza ahadi hiyo. Alianza kazi mara moja na ndani ya takribani siku 10 tulianza kuona kazi.
Ndani ya muda mfupi amefanya mambo muhimu ambayo yameanza kujibu maswali ya muda mrefu yaliyokosa majibu. Baadhi ya wananchi wamefurahishwa na hatua alizozichukua. Unaweza kuwaza kwanini mambo anayoyafanya Rais Magufuli yalishindikana hapo awali, yaani wakati wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne. Jibu ni rahisi tu, kulikuwa na uzembe, ubabaishaji, rushwa na ‘kupiga dili’ kulikofumbiwa macho kwa aina ya kipekee.
Jumatatu iliyopita Rais Magufuli alivunja Bodi ya Wakurugenzi ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), pamoja na kumuondoa madarakani Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Hussein Kidanto.
Alichukua hatua hiyo saa chache baada ya kufanya ziara ya kushtukiza ya kutembelea hospitali hiyo na kusikitishwa na taarifa ya kutofanya kazi kwa mashine za CT-SCAN na MRI kwa takribani miezi miwili huku mashine kama hizo zikifanya kazi katiuka hospitali za watu binafsi.
Aliuagiza uongozi wa Muhimbili ndani ya wiki moja mashine zote za uchunguzi wa magonjwa ziwe zinafanya kazi na ziwe zinahudumia wananchi inavyopaswa. Hapo napo Wizara ya Fedha ikakurupushwa na kutoa Sh3bilioni kulipia madeni ya matengenezo ya mashine hizo na nyingine nchini.
Tizama ajabu hii. Eti juzi mashine ya MRI imeanza kufanya kazi huku Muhimbili ikieleza kuwa mafundi wa Kampuni ya Philips ambao ndiyo wenye zabuni ya kufanya matengenezo vifaa hivyo, kukamilisha matengenezo ya kifaa hicho.
Haya ndiyo mambo ambayo wananchi walikuwa wakiyahitaji. Hakuna mwananchi anayefurahi kuona viongozi wa Serikali, wakikaa kimya wakati wao wanatesema kwa kukosa vipimo na tiba za kueleweka.
Ulijengeka uzembe na ubinafsi uliokithiri katika hospitali hii. Haiwezekani hospitali ya taifa ikose mashine hizi muhimu wakati hospitali binafsi zikiwa nazo, huku wagonjwa wakitakiwa kwenda kufanya vipimo katika hospitali hizo.
Kama tatizo lilikuwa deni la Sh3bilioni ina maana fedha hizo bila Dk Magufuli kuwa Rais zisingepatikana? Hii haiingii akilini, kuna uwezekano mkubwa baadhi ya watendaji wa hospitali hii walikuwa wakicheza dili na hospitali binafsi kwamba kila mgonjwa anayetoka Muhimbili akifanyiwa vipimo katika hospitali hizo za binafsi, wao ‘wanalamba mpunga’.
Tanzania ilipofikia sasa inahitaji rais makini maana siku hizi ni rahisi sana kwa Mtanzania kumuuzia Mtanzania mwenzake chakula kilichooza ama dawa zilizokwisha muda wake.
Ujanja ujanja, wizi, rushwa, ufisadi na udanganyifu umetamalaki nchini na kwa muda mrefu umefumbiwa macho jambo ambalo limetufikisha hapa tulipo.
Katika siku nne za kwanza, Rais huyu wa Serikali ya Awamu ya Tano pia alitoa maagizo kadhaa, ikiwamo kuitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuhakikisha inakusanya kodi hasa kwa kuwabana wafanyabiashara wakubwa, kuziba mianya ya ukwepaji kodi na kutangaza elimu bure kuanzia mwakani.
Pia alisema mabalozi wa Tanzania wanaowakilisha nchi huko nje, ndiyo watakaotakiwa kufanya shughuli zote kwenye nchi wanazofanya kazi hadi hapo atakapolitolea suala hilo uamuzi mwingine.
Kitendo cha Dk Magufuli kutaka TRA iwabane walipa kodi wakubwa na kuachana na utaratibu wa kuwabana walipa kodi ‘vidagaa’ linapaswa kuungwa mkono kwa sababu wafanyabiashara wakubwa ndiyo mabingwa wa kukwepa kulipa kodi.
Kama TRA ingekuwa inasimamia vyema ulipaji wa kodi bila kubagua vigogo na walalahoi ni wazi kuwa nchi isingekuwa na utegemezi katika bajeti kama uliopo sasa.
Hata katika matumizi ya magari ya Serikali kwa mawaziri na manaibu wao, wanapaswa kushushiwa rungu ili uwekwe utaratibu mwingine na si kutumia ‘mashangingi’ ambayo yana gharama kubwa kuyaendesha.
Agizo la kusitisha safari za nje hadi kwa kibali maalumu na kutaka shughuli ambazo zingefanywa na watendaji waliopo hapa nchini, zifanywe na mabalozi nalo linapaswa kuungwa mkono.
Hili litawafanya mabalozi kuwa na majukumu zaidi katika kuwakilisha nje, hapa tutapunguza matumizi makubwa ya nchi na kufanya fedha kuwa na matumizi katika masuala ya kusaidia vipaumbele vilivyopo.
Anachotakiwa kukifanya Dk Magufuli kwa sasa ni kuwa na kamati maalumu itakayofuatilia masuala nyeti yanayowagusa moja kwa moja wananchi.
Hata ‘figisufigisu’ tunazoziona bandarini, viwanja vya ndege, sekta ya madini, nishati, gesi, utalii na nyinginezo zinasababishwa na watu wachache wanaodhani kuwa Tanzania imeumbwa kwa ajili yao pekee.
Mambo mengi nchini yanakwama kwa kukosa usimamizi na ufuatiliaji tu. Hili la Muhimbili sidhani kama lilihitaji kuundwa tume, ni suala la kutoa agizo tu.
Kinachopaswa kufanywa na Serikali ya Awamu ya Tano ni kushughulikia kero za miaka zaidi ya 30 zinazowakabili wananchi. Haiwezekani nchi kila mwaka ina changamoto na matatizo yaleyale. Nani wa kuyatatua kama si Serikali iliyopo madarakani.
Wananchi hawakusanyi kodi, hawanunui mashine za CT-SCAN wala MRI. Kodi zao ndiyo zinazopaswa kutumika kununua vitu hivyo. Ni lazima Serikali ifanye kazi kwa ajili ya wananchi na si kwa kubebana na ushikaji. Spidi hii iendelezwe isiwe nguvu ya soda.





SOURCE:Mwananchi

































































Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

USAJILI WENYE MANUFAA EPL HADI SASA..