Mawaziri waapa bila shamrashamra...

Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano naWaziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makama akila kiapo.


Dar es Salaam. Halikuwa jambo la kawaida wakati hafla ya kuapishwa kwa mawaziri 30 Ikulu Dar es Salaam jana ilipofanyika kwa dakika 60, bila ya kuwapo kwa shamrashamra za aina yoyote.
Mawaziri hao waliokula kiapo mbele ya Rais John Magufuli, hawakuambatana na msururu wa wanafamilia ambao kwa kawaida hujazana kwenye viwanja vya jengo hilo jeupe kusindikiza wateule wanapoapa na baada ya kuapishwa huwavisha mashada ya maua kabla ya kuelekea kwenye sherehe nje ya Ikulu.
Jana, mawaziri hao walikwenda na ama mke, mume, mtoto au wazazi ambao hata hivyo hawakupewa fursa ya kupiga picha za kumbukumbu pamoja na Rais kama ilivyozoeleka.
Picha zilizopigwa ni tatu tu; ya kwanza ya Rais Magufuli na pamoja na mawaziri, ya pili ni naibu mawaziri na ya mwisho Rais alipiga na mawaziri wote na upigaji picha ulitumia dakika 20.
Baada ya kumaliza kupiga picha hizo, Dk Magufuli aliondoka huku mawaziri hao wakiitwa mmoja mmoja kupiga picha kwa matumizi maalumu na kisha kila mmoja kutangaziwa kuwa anatakiwa kuondoka, kila baada ya gari lake kuwa tayari langoni mwa jumba hilo la mkuu wa nchi.
Mawaziri hao waliondoka Ikulu kwa kutumia magari ya Serikali yaliyobandikwa namba za vibao vya wizara zao, huku kila mmoja akiondoka na mtu aliyekuja naye.
Katika hafla zilizopita za kuapishwa kwa mawaziri, Ikulu ilikuwa ikifurika kutokana na mawaziri kwenda na ndugu, jamaa, marafiki na familia zao na kisha baada ya picha ya pamoja na Rais, kila waziri alikuwa akipiga picha na kiongozi huyo mkuu wa nchi akiwa pamoja na familia yake na baada ya hapo wote walijumuika katika chakula na vinywaji.
Lakini hali ilikuwa tofauti jana, kwani hata juisi chache zilizoandaliwa kwa ajili ya wageni na mawaziri hao hazikunyweka. Kulikuwa na chupa za maji ya kunywa na glasi za juisi zilizoandaliwa kwa ajili ya kupoza makoo ya waheshimiwa hao, tofauti na hafla za kifahari zilizozoeleka kwenye viwanja vya Ikulu.
Mawaziri hao waliapishwa jana ikiwa ni siku moja baada ya kuteuliwa na Rais Magufuli ambaye aliapishwa Novemba 5 baada ya kushinda uchaguzi uliofanyika Oktoba 25.
Halfla hiyo iliyohudhuriwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan; Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa; Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue; Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, makatibu wakuu wa wizara na watumishi wa Ikulu, ilianza saa 4:58 asubuhi na kumalizika saa 5:58.
Tangu aingie madarakani, Rais Magufuli amepunguza matumizi katika hafla za kiserikali akielekeza fedha zaidi kwenye shughuli za kuhudumia wananchi.
Alianza kwa kufuta safari za nje za watumishi wa ummahadi kwa kibali maalumu cha Ikulu na baadaye kupunguza ukubwa wa sherehe ya kuwapongeza wabunge mjini Dodoma wakati akizindua chombo hicho na kuelekeza fedha za nyingi zitumike kununulia vifaa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Baadaye alitangaza kuwa sherehe za Uhuru wa Tanganyika zitumike kufanya usafi kote nchini na fedha zilizopangwa kwa ajili ya shughuli hizo ziende kuhudumia wananchi kabla ya kufuta sherehe za maadhimisho ya Wiki ya Ukimwi.






SOURCE:Mwananchi
































































Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

USAJILI WENYE MANUFAA EPL HADI SASA..