Mikataba ya viwanda, mashamba kuchunguzwa..
Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru.
Dar es Salaam. Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru amesema wameanza kuzipitia taarifa za utekelezaji wa mikataba ya viwanda na mashamba yaliyobinafsishwa baada ya kupokea kutoka kwa wawekezaji.
Licha ya kupokea taarifa hizo, amesema ofisi hiyo inaendelea kuchambua ripoti za maendeleo ya mashirika ya umma zilizopelekwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kama ilivyoagizwa.
Hatua hiyo imekuja baada ya Mafuru kutoa agizo Novemba 18 kwa wawekezaji wote waliopewa mikataba ya kuendeleza mali hizo, kuwasilisha taarifa zao ndani ya siku 30.
Katika agizo lake kwa wawekezaji hao, alisema ofisi yake kwa sasa inarejea mikataba yote ya mauzo ya viwanda na mashamba iliyoingiwa kupitia mpango wa ubinafsishaji.
Alisema kuna wawekezaji wamekiuka masharti ya mikataba yao, hasa ya kuendeleza mali hizo.
Jana, Mafuru aliiambia Mwananchi kuwa amepokea sehemu kubwa za taarifa hizo akieleza kuwa ni utaratibu wa kawaida kwa ajili ya kuandaa ripoti itakayosaidia wakati wa kikao na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) siku zijazo.
“Taarifa tulizozipokea ni nyingi sana na zinahusisha kiasi kikubwa cha ripoti za kifedha, hivyo timu yangu ya wachambuzi wanazipitia kufahamu kwa undani kinachoendelea huko na hili zoezi siyo la haraka kama watu wanavyofikiri,” alisema Mafuru.
Alipoulizwa iwapo kuna baadhi ya wawekezaji waliochelewa kuwasilisha taarifa hizo baada ya siku ya mwisho ya Desemba 18, alisema wapo kwa kuwa siku zote wachelewaji hawakosekani kama ilivyo shuleni.
Hata hivyo, hakueleza hatua zitakazochukuliwa kwa wale waliochelewa kuwasilisha taarifa kwa kuwa hivi sasa shughuli kubwa itakuwa ni uchambuzi wa taarifa hizo na muda ukifika wataujulisha umma.
Maoni
Chapisha Maoni