Mbeya kuanza kutekeleza agizo la Dk Magufuli..
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro.
Mbeya .Zaidi ya Sh3.5milioni zimetumika kununulia dawa kwa ajili ya wagonjwa wa virusi vya ukimwi Mkoani Mbeya ikiwa ni utekelezaj agizo la Rais Dk John Magufuli la kuzitaka fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya kufanya sherehe ya maadhimisho ya siku ya ukimwi dunia kununulia dawa.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro alisema kuwa fedha hizo zimetokana na michango ya wadau na taasisi mbali mbali ambapo baadhi yao walitoa vifaa tiba,Kanga,Tisheti na begi za shule.
Kandoro alifafanua kuwa kwa mujibu wa agizo kutoka kwa Rais Dk Magufuli hivyo Kanga,Tisheti na Begi za shule zilizotolewa na wadau zitapelekwa kwa walengwa ambao ni wagonjwa wa virusi vya ukimwi.
"Hakuna kitakachobadilika kila jambo litakwenda kama maagizo yalivyotolewa na Rais Dk Magufuli hivyo hizi dawa na vitu vingine namkabidhi mganga Mkuu wa Mkoa Seif Mhina ambaye ataandaa utaratibu wa kuvikisha sehemu husika kama tulivyokubaliana"alisema
Kandoro alisema kuwa jamii inapaswa kutambua kuwa bado kuna tatizo kubwa la maambukizi ya ugonjwa huo hivyo kila mmoja anawajibu wa kushiriki kikamilifu katika kupambana na maambukizi mapya ya VVU.
Awali akitoa taarifa ya maandalizi ya sherehe hiyo ambayo kimkoa ilitarajia kufanyika Rujewa Wilayani Mbarali Ofisa maendeleo ya jamii Mkoa Stella Kategelile alisema kuwa zaidi ya Sh32 milioni zilitarajiwa kutumika katika maadhimisho hayo.
Alisema maandalizi ya sherehe hizo yalianza Novemba 13,2015 ambapo shuguli mbali mbali zilifanyika ikiwa ni pamoja kutoa huduma ya ushauri nasaha na upimaji wa hiari ambapo watu 453 walipima na 34 walikutwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Seif Mhina alisema kuwa kuna vituo 78 vinavyo toa huduma kwa wagonjwa wenye VVU lakini kipaumbele cha kugawa na hizo kitakuwa kwenye vituo vyenye wateja wengi ambayo ni Hospitali ya Mkoa,Kituo cha afya Luanda,Igawilo na Kiwanja mpaka.
Maoni
Chapisha Maoni