Shein amweleza Rais Magufuli hatima ya Z’bar..
Rais John Magufuli akizungumza na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein (kushoto) Ikulu Dar es salaam jana. Picha na Mtandao wa Zanzibar.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli amefanya mazungumzo na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk Ali Mohamed Shein yaliyolenga kupatiwa mwenendo wa utatuzi wa mkwamo wa kisiasa ulitokea baada ya Uchaguzi Mkuu.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano, Ikulu iliyotolewa jana, Dk Shein alimweleza Rais Dk Magufuli kuwa utatuzi wa mgogoro chini ya kamati maalumu iliyopo chini yake, unaendelea vizuri.
Kamati hiyo iliyoanza kazi mapema Novemba 9, inawajumuisha pia Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Rais Mstaafu Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, marais wastaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Dk Salmin Amour.
Dk Shein alisema kuwa mazungumzo aliyofanya na Rais Magufuli yalilenga kumweleza hatma ya Zanzibar baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25.
Uchaguzi huo uliingia doa baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salim Jecha kutangaza kuufuta Oktoba 28 kutokana na kuvunjwa sheria na kanuni za uchaguzi visiwani humo.
Mgogoro huo uliodumu kwa takriban miezi miwili sasa unazidi kutengeneza sintofahamu visiwani humo ambako watu wake wamekuwa watulivu kipindi chote, kuliko miaka ya nyuma huku wakisubiri utatuzi.
“Kwa hiyo nimekuja kumpa taarifa mheshimiwa Rais Magufuli kuhusu maendeleo ya mazungumzo yetu ili aweze kujua kinachoendelea akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo Zanzibar ni sehemu yake, na sisi ni jukumu letu kumpa taarifa hiyo,” alisema Dk Shein.
Mara baada ya kupata muafaka, Dk Shein alisema kamati yake itatoa mrejesho kwa wananchi makubaliano hayo ambayo yamekuwa yakisubiriwa kwa muda, baada ya miezi miwili kupita bila kupatikana ufumbuzi wa kina.
Mazungumzo hayo ya jana yalifanyika zikiwa ni siku tano baada ya Maalim Seif kuteta na Rais Magufuli juu ya kutafuta suluhisho la mkwamo huo wa kisiasa.
Katika mazungumzo hayo ya Jumatatu, Rais alimwakikishia Maalim Seif kuwa Serikali itadumisha amani na utulivu visiwani humo.
Maalim Seif awali alikutana na Rais Jakaya Kikwete kabla ya hajamaliza muda wake Novemba, 5 na kufanya mazungumzo ambayo yaliweka mwelekeo mzuri wa kutafuta suluhu.
Mgogoro wa Zanzibar umezidi kuibua mashinikizo kutoka katika jumuiya za ndani na kimataifa kwa takriban miezi miwili sasa, wakitaka matakwa ya wananchi yasikilizwe. Tayari madhara ya shinikizo la kumaliza mgogoro huo yameanza kuonekana baada ya Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Maendeleo ya Changamoto za Milenia (MCC) la Marekani kuahirisha kutoa msaa wa Dola 472 milioni za Marekani (Sh992 bilioni) hadi hapo suluhu itakapopatikana.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga alisema hivi karibuni kuwa kinachoendelea Zanzibar kisiwe kigezo cha Jumuiya ya Kimataifa kudharau mafanikio ya kidemokrasia yaliyofikiwa nchini.
Aliitaka jumuiya hiyo kutambua utofauti wa siasa uliopo kati ya visiwani na bara na kwamba waendelee kuvuta subira wakati ya usuluhishi inaendelea kutatua mgogoro huo.
Maoni
Chapisha Maoni