Rais wa Chad apongeza utendaji Mahakama ya Afrika..
Rais wa Chad, Idriss Deby.
Arusha. Rais wa Chad, Idriss Deby amepongeza utendaji kazi wa Mahakama ya Afrika na Haki za Binadamu (AfCHPR) na kuahidi kuridhia itifaki ya kuanzishwa mahakama hiyo nchini humo.
Arusha. Rais wa Chad, Idriss Deby amepongeza utendaji kazi wa Mahakama ya Afrika na Haki za Binadamu (AfCHPR) na kuahidi kuridhia itifaki ya kuanzishwa mahakama hiyo nchini humo.
Rais Deby alitoa pongezi hizo alipokutana na Rais wa mahakama hiyo, Jaji Augustino Ramadhani katika Ikulu ya Chad jijini N’djamena.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na mahakama hiyo, Jaji Ramadhani alimshukuru Rais wa Chad kwa kutoa hakikisho la kuridhia itifaki hiyo.
Jaji Ramadhani aliongoza ujumbe wa mahakama hiyo kwenda Chad kufanya mikutano ya kujenga uelewa kwa taasisi za Serikali, wanasheria na tume za haki za binadamu kutoka Chad, Gabon, Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) na Jamhuri ya Afrika ya Kati. Tangu kusainiwa kwa itifaki ya kuanzishwa kwa mahakama hiyo mwaka 1998 ni nchi 29 tu kati ya 54 ambazo ni wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) zilizoridhia.
Pia, ni nchi saba pekee zilizotoa tamko la kuruhusu wananchi na asasi zisizo za kiserikali kufungua kesi zinazohusu ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya Serikali zao.
Nchi hizo ni Burkina Faso, Ivory Coast, Ghana, Malawi, Mali, Rwanda na Tanzania.
Taarifa hiyo ilisema tangu mwaka 2010 mahakama hiyo imekuwa ikifanya mikutano na makongamano ya mara kwa mara barani Afrika ili kujitangaza.
Ilisema lengo ni kujenga uelewa kwa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) kujua namna ya kuitumia mahakama hiyo ili kulinda haki za binadamu katika nchi zao.
“Lengo jingine la mikutano hiyo ni kuitambulisha mahakama kwa wananchi na asasi zisizo za kiserikali ili kuitumia pindi wanapoona haki za binadamu zimekiukwa,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza kuwa hadi sasa mikutano 24 imeshafanyika.
Maoni
Chapisha Maoni