Profesa Muhongo anusa rushwa Rea mkoani Kagera..

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa SospeterWaziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo      

Bukoba. Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amenusa rushwa katika Wakala wa Umeme Vijijini (Rea) ya njia za uunganishaji umeme zinazochepushwa, huku taasisi za dini na wananchi wakitozwa fedha kinyume cha utaratibu ili waunganishiwe nishati hiyo.
Kutokana na kubaini hilo, Profesa Muhongo ameiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza suala hilo, akisema amepokea malalamiko mengi ya wananchi na kutoa mfano wa Wilaya ya Muleba mkoani Kagera ambako kanisa moja lilitakiwa kutoa rushwa.
Alisema wananchi wanatozwa kiasi kikubwa cha fedha tofauti na maelekezo na kuagiza waanze kupewa elimu ili wafahamu taratibu za kufuata kabla ya kuunganishiwa umeme.
Profesa Muhongo aliutaja Mkoa wa Kagera kuwa unaongoza kwa malalamiko.
Akiwa mjini Bukoba baada ya ziara yake ya siku mbili, alizionya kampuni zilizopewa kandarasi ya kusambaza umeme na kulalamikiwa na wananchi kuwa Serikali itaachana nazo.
Alisema vitendo vya rushwa vimedaiwa kusababisha kuchepushwa kwa maeneo mengi ambayo hayakuwa kwenye ramani na kusababisha walengwa kukosa nishati hiyo.
Hata hivyo, Profesa Muhongo aliagiza waliopelekewa miundombinu ya umeme kwa makosa wasinyang’anywe.
Mkandarasi anayesimamia usambazaji wa umeme vijijini mkoani Kagera kupitia Rea, Julius Kateti alidai viongozi wa kisiasa hasa madiwani huwatoza wananchi kiasi kikubwa cha fedha tofauti na kiwango halisi cha Sh27,000.
Meneja wa Tanesco Kada ya Ziwa, Amos Maganga alithibitisha tatizo hilo pia kuikumba mikoa ya Geita, Mara na Simiyu, huku Meneja wa shirika hilo mkoani Kagera, Hassan Said akisema makandarasi wanatoa mikataba ya muda mfupi hali inayochangia rushwa na uhamishaji wa nguzo.     






SOURCE:Mwananchi


































































































Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

USAJILI WENYE MANUFAA EPL HADI SASA..