Shambulizi la kigaidi Mandera.
Waziri wa usalama wa ndani wa Kenya Joseph Nakaisery amewasifu abiria waislam waliokuwa kwenye basi la kampuni ya Makkah kwa kuwalinda wenzao wakristo mbele ya kundi la al-Shabab Jumatatu.
Aliongeza kuwa al-Shabab bado ndio washukiwa wakuu wa shambulizi hilo la Mandera .
Watu wawili walifariki dunia katika shambulizi hilo la Jumatatu Kaskazini mwa Kenya Mandera ambapo washambuliaji wanaaminika kuwa ni wanamgambo wa al-Shabab.
Kwa mujibu wa mashahidi wa tukio hilo waliona abiria waislam wakiwapa hijab wenzao wa kikristo ili wasijulikane kama ni wakristo mbele ya wanamgambo hao.
Na maafisa wa eneo hilo wanaeleza kwamba wanmgambo hao walitoa amri kwa abiria kujipanga katika makundi mawili wakristo na waislam lakini abiria hao walikataa kufanya hivyo wakisema kama wanataka wawauwe wote kwa pamoja.
Akizungumza na VOA Swahili mchambuzi wa masuala ya kisiasa na jamii nchini Kenya Baraka Muluka ameeleza hiki ni kitendo cha kutia moyo sana kuonyesha wakenya wameweza kushirikiana na kuona huyu si adui wa wakristo au waislam pekee ni adui wa wote jambo ambalo linaweza kusaidia kupiga hatua zaidi , kwa sababu gaidi ni mtu ambaye anatumia vibaya dini ya kiislam ili kutimiza malengo yake machafu alisema.
Shambulizi jingine kama hilo lilitokea mwaka jana ambapo wanamgambo wa al-Shabab waliuwa watu 28 wasio waislam walioshushwa kwenye basi ambapo waliwekwa makundi mawili na waislam kuachiwa huru.
SOURCE:VOA
Maoni
Chapisha Maoni