Dk Magufuli ana mtihani ndani ya CCM..
Rais John Magufuli.
CCM imevuka vikwazo vyote katika Uchaguzi Mkuu uliomalizika Oktoba, lakini bado haijamaliza kazi. Kazi ya kutetea utawala wake ndiyo pekee iliyomalizika, lakini imeanza kazi ya kuhakikisha inautetea katika uchaguzi ujao.
Kazi hiyo ina vikwazo. Bado vikwazo vingi haijavivuka ambavyo ndivyo vitatoa taswira ya namna gani chama hicho kikongwe barani Afrika kitakamilisha salama ng’we ya miaka mitano ijayo kabla ya uchaguzi mwingine.
Vikwazo vingi vimetajwa. Vingi vimesikika, lakini pia vipo ambavyo havijatajwa wala kusikika, hivyo ni vile vya ndani. Vile ambavyo hata wanaCCM wanaovijua ni wachache na ni wale tu walio katika nafasi za juu za uongozi ndani ya chama hicho.
Chama hicho chini ya uenyekiti wa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete kina makundi. Yapo makundi ya aina mbalimbali, lakini ni yale ya walionufaika na mchakato uliomwingiza Dk Magufuli madarakani na wale waliojiweka au kuwekwa kando wakati wa mchakato wa urais.
Kundi la walionufaika na mchakato huo litaendelea kuwapo na ni hilo linalojitia hivi sasa kuwa karibu naye, ilhali lile lililowekwa kando linaendelea kunung’unika. Hata hivyo, ukubwa wa kundi hilo la pili ni tishio kwa Serikali mpya katika siku za usoni kwa sababu ndilo lililotaka kukimega chama hicho wakati wa mchakato huo, likiungana na lile lililokuwa likimuunga mkono mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa ambalo miongoni mwa mwao aliondoka nao alipojitenga na chama hicho.
Miongoni mwao ni wale waliowahi kuwa makatibu wa mikoa, wilaya na idara mbalimbali za ndani ya chama hicho ambao waliondolewa madarakani katika mazingira ambayo hayawakuwaridhisha, baadhi yao wakiwa wale walioamua kuondoka wakiwamo waliowekwa benchi.
Hadi sasa, kundi hilo lina washirika wake ndani ya CCM na nguvu kubwa ambayo iwapo Serikali ya Dk Magufuli haitafanya kazi ipasavyo na kupata uungwaji mkono wa kutosha wa wananchi, linaweza kukiathiri chama hicho katika chaguzi mbalimbali zijazo na hata Uchaguzi Mkuu wa 2020.
Kundi la Wahafidhina
Ndani ya makundi niliyotaja hapa juu, limo kundi la wahafidhina. Mara zote wahafidhina ni watu wasiokubali mabadiliko na kwa aina ya utendaji wa Serikali ya Dk Magufuli inayofanya mambo mengi ambayo hayakufanywa na watangulizi wake, hakika kundi hilo halifurahishwi nayo, hususan yale ambayo pia yanakiumbua chama hicho.
Wahafidhina hao walijijengea mazingira na fursa za kunufaika na chama hicho kutokana na kuwamo ndani ya CCM.
Hao ndiyo waliojipatia majina makubwa na ni ambao walitembea vifua mbele wakitambia kuwamo ndani ya chama hicho tawala.
Kutokana na mabadiliko yanayoonekana ya kiutendaji na udhibiti wa mali na rasilimali za Taifa kunakofanywa na Serikali iliyopo madarakani, kundi hilo linaona mianya na fursa lilizokuwa nazo kana kwamba zinaondoka polepole na hatimaye mbele ya safari halitakuwa na chochote.
Hali hiyo inawafanya wahafidhina hao wawe tayari kukwamisha harakati zozote zitakazoanzishwa na Dk Magufuli, hususan ndani ya chama chake pale atakapokabidhiwa uongozi wa chama hicho.
Pia, hata zile zitakazohitaji msaada wa chama chake kabla ya wakati huo zinaweza kukwamishwa.
Kundi la watendaji wabovu
Kuna kundi la watendaji dhaifu au wabovu ambao CCM imewalea kwa miaka mingi. Watendaji hao wamo ndani ya chama hicho na wamekuwa wakitekeleza majukumu yao kwa mtindo wa ‘bora liende’.
Bahati mbaya ni kuwa miongoni mwa watu hao wana nguvu ambazo zinaweza kuutikisa mfumo wa uongozi wake ndani ya chama hicho pale atakapokadhiwa uongozi.
Yapo madai kuwa wakati wa mchakato, udhaifu wa watendaji hao wakiwamo baadhi ya makatibu wa wilaya na mikoa, ulichangia kuimarisha upinzani katika maeneo ya uongozi wao na kuvisaidia vyama vinavyounda Ukawa kushinda ama viti vingi vya udiwani na ubunge au kukusanya kura nyingi za urais.
Aidha, ni hao miongoni mwao ambao udhaifu wao ulikifikisha chama hicho mahali ambako upinzani ulikuwa ukitamba katika maeneo wanayoyaongoza kana kwamba hawakuwapo.
Hata hivyo, Dk Magufuli atakuwa na kazi ngumu kuwang’oa watu hao madarakani, ikizingatiwa kuwa baadhi yao wana mizizi iliyojiimarisha.
Naamini kwamba iwapo ataichukua CCM na kuamua kuiongoza kwa ‘staili’ anayoitumia kuongoza Serikali kwa sasa, ile ya kila mmoja awajibike kazini, watendaji hao masilahi wanaotaka chama hicho kiwatumikie badala ya wao kukitumikia, watakigawa. Swali ni je, atakabiliana nao vipi? Ni suala la kusubiri.
Miradi ya chama
Suala jingine ni lile la miradi ya chama hicho ilivyochoka. Miradi mingi ya kiuchumi ya CCM imechoka na mingine imechoshwa na watendaji.
Wakati akizindua jengo jipya la ukumbi wa mikutano ya CCM mjini Dodoma, Rais mstaafu na mwenyekiti wa chama hicho, Kikwete alikemea tabia ya watendaji kugeuza miradi kuwa sawa na mali yao, badala ya kuwatumikia wanachama.
Kikwete aliwataka viongozi wa chama hicho kuwa wabunifu akitoa mfano wa baadhi ya viwanja vya chama hicho ambavyo miongoni mwao wamejimilikisha, miradi imeporwa, majengo yamekodishwa kwa hadi miaka 30 ijayo na maeneo mengi hasa mijini ikiwamo Dar es Salaam yaliyogeuzwa kuwa maegesho ya magari, badala ya kuendelezwa kibiashara zaidi.
Ipo pia miradi mingine ya chama hicho imeuzwa na watendaji hao kwa bei ya kutupa.
Waliofanya hayo wanamsubiri kwa ‘hamu’ Dk Magufuli wakabiliane naye, maana siamini kama watakuwa tayari kuona wakipokonywa tonge mdomoni, ilhali wamejimilikisha utajiri.
Dira ya chama
Hili ni eneo jingine atakalokabiliana nalo ambalo huenda likamtesa. Uwapo wa Ukawa unaifanya CCM isilale, ijione kuwa inalo jukumu kubwa la kuwatumikia wananchi ipasavyo na kuridhisha matakwa yao.
Kwa ufupi ni kuwa CCM inakumbana na upinzani mkali hivi sasa na inavyokwenda inapaswa kuwa dira.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana walau amekifufua baada ya watangulizi wake kukichakaza kiasi cha kufifisha taswira yake kwa jamii.
Hata hivyo, bado kinazongwa na upinzani unaoimarika na ulioimarishwa na makada waliokihama ambao wanaendelea kujipanga kwa ajili ya kupambana nacho wakiamini kwamba walichopoteza ni pambano, lakini siyo mchezo.
Je, falsafa ya chama hicho kuanzia sasa na hata Dk Magufuli atakapokabidhiwa ni ipi? Itakuwaje? Itabaki kuwa chama cha wanyonge au wachache?
Walio madarakani au wakulima na wafanyakazi kama ilivyo nembo yake? Kwa vyovyote vile hii ni kazi inayomsubiri Dk Magufuli.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wanaiona CCM chini ya mwenyekiti mpya ajaye, Dk John Magufuli kuwa ni chama kinachoweza kuibua upya tumaini la Watanzania hasa baada ya kuonekana kupoteza dira katika miaka ya hivi karibuni.
Kwa nyakati tofauti wachambuzi hao wamebainisha kuwa Watanzania wameichoka CCM kutokana na tabia iliyoanza kujengeka ya kuwakumbatia watu wenye fedha na viongozi na kuwasahau walalahoi ambao ndiyo iliyokuwa falsafa ya chama hicho tangu kuanzishwa kwake na marehemu Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.
Maoni
Chapisha Maoni