Wakazi 600 wahangaikia kulipwa fidia baada ya kutakiwa kuhama kupisha ujenzi wa bandari Tanga..
Wakazi zaidi ya 600 waliopo kata ya Magaoni jijini Tanga wameiomba serikali kuingilia kati kufuatia kuhangaikia kulipwa fidia ya mashamba na nyumba zao baada ya kuamriwa wahame ili kupisha ujenzi wa miundo mbinu ya ujenzi wa bandari mpya ya Mwambani iliyopo jijini Tanga.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara waliotayarisha viongozi wa serikali ngazi za mitaa na kata, waathirika hao wamesema awali miaka miwili iliyopita walilipwa kiasi kidogo cha fidia na kampuni hodhi ya raslimali za reli nchini (RAHCO) kisha baadae wakaahidi kuwa kama kuna makosa yaliyojitokeza kulingana na tathmini iliyofanywa na wataalam husika ikilinganishwa na viwango vya fedha walivyolipwa vitarekebishwa lakini hadi leo hakuna utekelezaji.
Wakifafanua tathmini iliyofanywa na viwango walivyopewa baadhi ya waathirika hao wamesema kulikuwa na mkanganyiko baina ya wathamini wa halmashauri ya jiji na viongzoi wa (RAHCO) hatua ambayo aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Tanga enzi hizo Halima Dendego aliingilia kati na kuhakikisha kuwa viwango vilivyowekwa vinawiana na mali za waathirika ikiwemo nyumba na mazao yaliyokuwa shambani.
Hata hivyo mkuu wa wilaya ya Tanga Bwana Abdulla Lutavi amekataa kurekodiwa akidai kuwa hawezi kuzungumzia lolote kuhusu madai ya wakazi hao hadi hapo watakapowasilisha malalamiko rasmi ofisini kwake.
SOURCE:ITV
Maoni
Chapisha Maoni