Chadema kuwasha moto nchi nzima..
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji Picha na Mtandao
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinatarajia kuanza mikutano ya hadhara na ya ndani nchi nzima ili kujenga na kuinua uhai wake kuanzia Juni mwaka huu.
Hiyo itakuwa mara ya kwanza kwa Chadema kufanya mikutano tangu baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana ambayo inalenga kukijenga na kuamsha ari ya wanachama tangu kilipokosa kura za kutosha kukiwezesha kushika dola.
Miaka ya nyuma, Chadema ilipata umaarufu kupitia mikutano iliyopewa majina Operesheni Sangara na Vuguvugu la Mabadiliko (M4C).
Akizungumza na waandishi wetu juzi alipofanya ziara katika ofisi za gazeti hili zilizopo Tabata, Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji alisema wapenzi wa chama hicho wakae mkao wa kusubiri mikutano iliyoandaliwa nchi nzima katika ngazi ya kanda.
“Kuanzia mwezi ujao tutaanza kuhakikisha watu hawasinzii. Kutakuwa na mikutano ambayo itakuwa inaratibiwa na kanda. Itategemea uzito wa ajenda ya hiyo kanda kisha watatujulisha sisi huku juu kama sekretarieti,” alisema Dk Mashinji.
“Kutakuwa na kazi nchi nzima, yale mambo ya kusema (Mwenyekiti wa Chadema Freeman) Mbowe yuko wapi leo hayatakuwepo tena. Kama ni Mtwara watakuwa huko na gesi yao, Bukoba watakuwa wanapambana na kahawa… nchi yote itakuwa kazini kwa sababu sisi tumegatua madaraka mikoani,” aliongeza.
Alipoulizwa watakuwa na ajenda gani baada ya ile ya ufisadi iliyowapa umaarufu kuporwa na Serikali ya Rais John Magufuli, Dk Mashindi alisema chama hakiendeshwi kwa ajenda za matukio, tu bali kwa itikadi na falsafa.
“Sidhani kama chama cha siasa kinaendeshwa kwa ajenda za matukio… Chama cha siasa kinaundwa na itikadi na falsafa. Hakipo kusubiri chama tawala kikosee ndipo kipate gia. Chama cha siasa kina kazi ya kueneza itikadi yake. Hapo ndipo mimi nataka kusimamia,” alisema.
Alipoulizwa kama atamudu kuvaa viatu alivyoviacha mtangulizi wake, Dk Willibrod Slaa, Dk Mashinji alijibu; “Viatu vya Dk Slaa, viko wapi nivipime? Wakati mwingine unamwangalia mtu anasema viatu vya Dk Slaa vikubwa, lakini mimi ndiye niliyekuwa injini yake. Najua unaweza kuwa injini ya mtu lakini ukipewa ile nafasi usiweze kufanya. Lakini ni kashfa gani aliyolipua Dk Slaa utakayouliza ambayo hatukuifanyia kazi?” alihoji.
Dk Mashinji alisema anaamini nafasi hiyo anaimudu. “Kwa asili binadamu huwa wanapenda kulinganisha watu. Dk Slaa alifanya mambo kwa wakati wake na mimi nitafanya kwa wakati wangu kuimarisha Chadema kuwa na uwezo kama taasisi,” alisema.
Akizungumzia hatua mbalimbali ambazo Chadema imepitia, Dk Mashinji alisema mikakati yao ni kukijenga chama kuanzia ngazi za chini na kutekeleza ahadi za wananchi katika majimbo, manispaa na halmashauri wanazoziongoza.
“Ukiangalia kama chama tunakwenda kwenye mabadiliko ya siasa na sasa tuko kwenye hatua muhimu sana. Tunaongoza halmashauri 24, hatuwezi kuendelea kuwa walalamikaji, bali watendaji,” alisema.
Alisema tangu walipokisajili chama hicho Januari 14, 1993 na kupewa hati ya usajili, kazi kubwa ilikuwa kujenga msingi. “Mwaka 1995 tuliweka wagombea wachache wa ubunge kwa sababu chama ndiyo kilikuwa kinakua. Tulipofika mwaka 2005 tukasema hapana. Lazima tukitangaze chama. Unapotangaza lazima pia ukiuze, tukamweka Mbowe. Akawa Mzee wa helikopta, akazunguka nchi nzima, ndiyo Chadema kikawa ndani ya watu,” alifafanua.
Alisema mwaka 2006, walianzisha programu ya Chadema ni Msingi iliyolenga kutoa elimu ya uraia. “Programu hiyo ilivuta watu wengi wakiwamo hata wa nje. Hapo ndiyo mlisikia ‘Chadema wanapewa hela na watu wa nje kutuoandoa madarakani’. Hapana, ilikuwa elimu ya uraia kabisa. Unawafundisha wananchi sheria za chama, Katiba inasemaje, huzungumzii chama hapo. Hiyo ni siku ya kwanza,” alisema.
Alisema siku ya pili walikuwa wakiitumia kuwafundisha Chadema ni nini, itikadi yao pamoja na mrengo wao.
“Sisi ni mrengo wa kati; kama unakuja na ubepari au ukomunisti hatujali. Falsafa yetu ni Nguvu ya Umma. Hata ukiangalia Katiba ndivyo inavyosema. Huwa tunasema tutawashtaki kwenye mahakama ya wananchi, kwa sababu ndiyo mahakama ya juu.”
Dk Mashinji alisema operesheni hii ya sasa itaendelea hadi mwaka 2019 wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili waweze kushinda na kujiandaa kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
“Tunapokwenda kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, sera zitaonyesha kuwa hiki chama kimefikia hatua ya kushika dola,” alisema.
Source:Mwananchi
Maoni
Chapisha Maoni