Wafanyakazi wamtwisha JPM mzigo kwa mambo 10..
Rais John Magufuli
Wakati wafanyakazi duniani wakisherehekea Sikukuu ya Mei Mosi leo, wenzao wa Tanzania wamemtwisha Rais John Magufuli mzigo wa hoja 10 wanazoamini zitawaboreshea maisha, kupunguza migomo na kuleta ufanisi kazini.
Hoja hizo zimetolewa siku moja kabla ya Rais Magufuli kushiriki kwa mara ya kwanza kwenye maadhimisho hayo mjini Dodoma, huku kukiwa na kiporo cha ahadi za mtangulizi wake, Jakaya Kikwete za kuboresha masilahi yao.
Kwa nyakati tofauti, Rais Magufuli anayetimiza miezi sita akiwa Ikulu wiki hii, amekuwa akiahidi kuboresha maisha ya wafanyakazi kwa kupunguza kiwango cha makato ya kodi ya mapato kwa wafanyakazi, kuongeza mishahara na kudhibiti ajira za wageni kupitia operesheni maalumu.
Akizungumza na mwandishi wetu jana, Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Hezron Kaaya alisema kupitia maadhimisho hayo wanategemea kusikia majibu ya hoja mbalimbali zinazoendelea kuwakandamiza wafanyakazi nchini.
Mosi, Kaaya alisema kima cha chini kwa mfanyakazi kwa sasa kinatakiwa kuwa Sh750,000 ili kuweka uwiano wa kipato na gharama za maisha, hivyo kama anahitaji kupambana na ufisadi, lazima aimarishe mishahara ya wafanyakazi nchini.
“Jambo la pili ni kuunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii ili tuwe na mfuko mmoja wa hifadhi ya umma na mwingine wa sekta binafsi ili kuondoa malalamiko yanayojitokeza kwa wastaafu.”
Hata hivyo, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano, Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Sarah Kibonde alisema tayari majadiliano ya kuunganisha mifuko hiyo yameshaanza katika hatua za awali na kwamba jambo hilo linahitaji ushiriki wa Serikali, waajiri na wafanyakazi akisema mazungumzo na pande hizo yameanza.
“Ni sawa na maandalizi ya kupika chakula, ndiyo bado kabisa kibichi kwa sababu jambo linagusa hisia sana.”
Mbali na hilo, Kaaya alimwomba Rais Magufuli kudhibiti na kulinda kikamilifu ajira za Watanzania dhidi ya wageni. Kaaya alizungumzia mishahara hewa na kuishauri Serikali kumaliza changamoto hiyo kwa kuangalia chanzo chake.
“Kuna wafanyakazi wengi wanapangiwa kazi lakini hawaendi kuripoti kwa sababu ya mazingira mabovu, mishahara inabakia wazi na inasababisha mwanya wa mishahara hewa,” alisema.
Jambo la nne, Kaaya alisema anatarajia pia Rais Magufuli kupitia Serikali yake, ataweka mazingira ya kulinda ajira za ndani kwa sababu sheria ya udhibiti wa ajira kwa wageni haifanyi kazi, hivyo angetamani kusikia tamko la mkuu wa nchi.
Kuhusu hoja ya kupunguza mishahara kwa vigogo wa mashirika, kiongozi huyo wa wafanyakazi alipingana na uamuzi huo akisema Rais alitakiwa kuvunja mikataba yao ili kuanza upya.
“Hawakujiwekea wenyewe ongezeko hilo, walijadiliana na bodi, wakapitisha kwa hiyo huwezi kufika mahali uamue tu kuwapunguzia. Lakini kwa kuwa ameona ni tatizo, alitakiwa kuvunja mikataba yao,” alisema.
Kaaya alitaja jambo la sita wizara inayohusika na masuala ya kazi kuongezewa nguvu ya bajeti kwa ajili ya kukidhi changamoto mbalimbali za ajira.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (Trawu), Mussa Kalala alisema mbali na hoja hizo, anatamani Rais Magufuli apunguze kiwango cha makato ya kodi ya mapato kwa wafanyakazi kutoka asilimia 12 hadi tisa au nane ili kumpunguzia mfanyakazi ukali wa maisha.
Tayari Rais Magufuli amesema anakusudia kupunguza kodi hiyo hadi kuwa tarakimu moja ili kupunguza mzigo kwa mfanyakazi na badala yake kubuni vyanzo vingine vya mapato.
“Lakini jambo jingine ni kwamba Serikali inatakiwa ilipe deni la mifuko ya hifadhi ya jamii ili wastaafu waweze kupata fedha zao, wastani wa asilimia 50 ya Deni la Taifa linatokana na mikopo ya mifuko hiyo, matokeo yake mifuko inashindwa kujiendesha, kwa mfano GEPF,” alisema.
Wachambuzi wa masuala ya kiuchumi wamekuwa wakikosoa kiwango cha mishahara kutokuakisi hali halisi ya mahitaji ya sasa katika mazingira wanayoishi huku Serikali ikitakiwa kutumia kigezo kikuu cha kupanda kwa gharama za maisha ili kuangalia itaongezaje viwango vipya vya mishahara.
Profesa Humphrey Moshi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema pamoja na kuzuia safari za nje, kudhibiti mishahara hewa na kuokoa kodi zinazopotea, Rais Magufuli anatakiwa kupunguza gharama zisizokuwa za lazima kwa mawaziri kwani wanaweza kujilipia umeme na maji kwa mishahara yao.
Mtafiti huyo wa masuala ya kiuchumi, alipendekeza pia kuunda chombo cha kusimamia mishahara ya sekta ya umma na kuanzisha sera ya mishahara itakayoweka vigezo vya mishahara kwa watumishi wake.
Maoni
Chapisha Maoni