TAKUKURU yabaini kuwepo kwa tani za sukari 4,579.2 katika Maghala ya Mbagala na Tabata jijini Dar es Salaam.


Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa inafanya uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazowahusu wafanyabiashara wa sukari nchini kwa kuficha bidhaa hiyo ili  kusababisha upungufu katika soko na hivyo kuleta usumbufu kwa jamii ya watanzania wanaohitaji bidhaa hiyo kwa matumizi jambo ambalo limesababisha kupanda kwa bei hadi kufikia shilingi elfu nne kwa kilo moja ya sukari.

Taasisi imeanza uchunguzi dhidi ya Tuhuma hizi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na tayari tumeweza kutembelea Maghala ya mfanyabiasha Haruni Daudi Zacharia ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Al-Naeem yaliyoko Mbagala na Tabata ambaye ni miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa nchini wa sukari na anayetuhumiwa kuficha bidhaa hii. 
 
Mnamo tarehe 05 Mei, 2016 timu ya uchunguzi ilitembelea maghala ya Tabata na kubaini uwepo wa sukari yenye jumla ya tani 4,579.2 iliyonunuliwa toka Kiwanda cha Kilombero Sugar Company.

Aidha uchunguzi ulibaini kuwepo kwa njama za dhati za kutouza kwa sukari kulikofanywa na mfanyabiashara huyu kwani hata sehemu ya Maghala ilipo sukari hapakuwepo dalili za upakiaji wa sukari na baada ya kufika Kitumbini tulibaini uwepo wa wananchi wengi waliokuwa wakihitaji bidhaa hiyo na wachache sana waliweza kuuziwa tena kwa kiwango kidogo sana kuliko mahitaji yao. Wananchi wengi walikosa huduma hiyo licha ya ukweli kwamba sukari ilikuwepo.
 
Uchunguzi uliofanyika umebaini kuwepo kwa mikakati ya dhati iliyokuwa ikifanywa na mfanyabiasha huyu kwa kununua sukari yote toka viwanda vya ndani na kisha kuihifadhi na kuuza bidhaa hiyo kidogo kidogo kwa wastani wa tani 250 kwa siku wakati alikuwa na uwezo wa kuuza zaidi jambo lililochangia uhaba wa sukari katika soko. 

Kuficha bidhaa ni kosa la uhujumu uchumi na ni  kinyume na Aya ya 3 Jedwali la kwanza Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 [Chapisho la Mwaka 2002]. Serikali haitavumilia hujuma za namna hii na itachukua hatua kali dhidi ya mfanyabiashara yeyote ataekwenda kinyume na sheria hii.
 
Kuanzia sasa TAKUKURU inatoa wito kwa wafanyabiashara wote wa sukari kuacha vitendo vya kuficha sukari na vyombo vya uchunguzi vinafuatilia kote nchini na yeyote atakayebainika kufanya hujuma hizo atakabiliwa na mkondo wa Sheria.
VALENTINO MLOWOLA MKURUGENZI MKUU WA TAASISI YA KUZUIA NA KUPAMBANA NA RUSHWA.



Source:ITV















































































































Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

USAJILI WENYE MANUFAA EPL HADI SASA..