Daktari asimamishwa kazi kwa uzembe uliosababisha kifo Mkoani Mara.
Uongozi wa halmashauri wa wilaya ya Butiama mkoani Mara umemsimamisha kazi daktari mwandamizi wa hospitali wa Wilaya hiyo na kutoa onyo kali kwa mtaalam mmoja wa maabara baada ya kudaiwa kufanya kazi kwa uzembe hatua ambayo imesababisha kifo cha mtoto Stephen Julius mwenye umri wa miaka minne mkazi wa kijiji cha Butiama.
Kusimamishwa kwa daktari huyo Dk Henri Japhat Msusa kunafuatia tume iliyoundwa na uongozi wa hospitali hiyo muda mfupi tu baada ya mtoto huyo afariki dunia na maelezo ya uzuni na kina ambayo yametolewa na mama mzazi wa mtoto huyo Bi.Pilly Juma James, mbele ya mkuu wa mkoa wa Mara Bw Magesa Mulongo katika mkutano wa hadhara ambao umefanyika kijijini Butiama.
Akitoa taarifa ya uchunguzi wa tume iliyoundwa na uongozi wa hospitali hiyo ya Butiama na sababu ambazo zimesababisha kifo cha mtoto huyo,Mganga Mkuu wa halmashauri ya Butiama Dk Archard Rwezahura, amesema mbali na mtoto huyo kusumbuliwa na malaria kali,lakini uzumbe ambao umefanywa na watumishi hao umechangia kifo cha kijana huyo kwa kushindwa kumpa huduma kwa zaidi ya saa nane tangu alipofikishwa katika hospitali hiyo.
Kufutia taarifa hiyo ya uchunguzi ambao umefanywa na timu ya madaktari wa hospitali hiyo,mkuu huyo wa mkoa wa mara Bw Magesa Mulongo,amemuagiza mkuu wa wilaya ya Butiama kufikisha taarifa hiyo kwa jeshi la polisi na TAKUKURU ili uchunguzi wa kina ufanyike na endapo itabainika watumishi hao walifanya uzembe na kusabisha kifo, hatua kali za kisheria zikuliwe dhidi ya watumishi hao.
Source:ITV
Maoni
Chapisha Maoni