Afrika Kusini waishinda Argentina katika raga
Afrika Kusini walijilinda vyema dhidi ya mashambulio ya Argentina.
Afrika Kusini imemaliza nambari tatu katika Kombe la Dunia la Raga baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya Argentina.
Afrika Kusini walikuwa wakiongoza kwa pointi 16-0 kufikia wakati wa mapumziko kupitia trai ya JP Pietersen na bao la Handre Pollard kabla ya Nicolas Sanchez kuwazolea Pumas pointi za kwanza.
Lakini trai ya Eben Etzebeth iliwaweka Boks mbele sana na pointi za Juan Pablo Orlandi alizozizoa dakika za mwisho hazikuweza kuwarejesha Argentina kwenye mchezo.
Masikitiko pekee kwa Boks ni kwamba Bryan Habana hakuweza kutwaa tena rekodi ya kufunga trai nyingi zaidi katika Kombe la Dunia.
Winga huyo wa umri wa miaka 32 alikaribia sana kufunga kipindi cha kwanza lakini akazuiwa na mkabaji kamili wa Argentina Lucas Gonzalez Amorosino.
Afrika Kusini walitumia kikosi chao bora cha kwanza na ubabe wao ulidhihirika wazi katika mechi hiyo iliyochezewa mashariki mwa London.
Argentina walidhibiti mpira sana lakini walipata ngome ya Afrika Kusini ikiwa imelindwa vyema kila walipojaribu kushambulia.
Macho sasa yanaelekezwa kwa mechi ya fainali kati ya New Zealand na Australia hivi leo.
SOURCE:BBC
Maoni
Chapisha Maoni