Serikali kuwalipa wafanyakazi wa MPM..

 Mgombea mwenza wa urais wa CCM, Samia Suluhu
Mgombea mwenza wa urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan akihutubia wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Viwanja vya Mlowo, Jimbo la Mbozi mkoani Mbeya, juzi. 
Iringa. Baada ya vuta nikuvute ya miaka 10 kati ya Serikali na waliokuwa wafanyakazi wa Mufindi Paper Mills (MPM), kuhusu malipo ya fidia yao, hatimaye Serikali imekubali kulipa fedha hizo kiasi cha Sh3.7 bilioni.
Wafanyakazi hao zaidi ya 700 waliahidiwa kulipwa fidia hiyo jana ikiwa ni moja ya ahadi walizopewa wakazi wa Kata ya Mtwango katika Jimbo la Mufindi Kusini na mgombea mwenza wa urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan.
Alisema serikali ijayo mara itakapoingia madarakani, itahakikisha inawalipa wafanyakazi hao fedha zao. “Ninafahamu mgogoro huu ni wa muda mrefu, ninawaahidi tutakapoingia madarakani tutaumaliza na tutalipa fidia kwa wafanyakazi wote,” aliahidi Samia na kuongeza:
“Hatuwezi kuwaacha wananchi wetu waumie wakati sisi tupo.”
Samia alitoa ahadi hiyo baada ya kuelezwa changamoto zinazowakalibi wafanyakazi hao, ikiwamo ya kudai fidia yao na mgombea ubunge wa Mufindi Kusini, Mendrad Kigola.
Kigola alisema tangu kiwanda hicho kilipobinafsishwa na Serikali mwaka 2005 na kupewa muwekezaji, wafanyakazi hao hawajilipwa fidia zao hadi sasa.
Alisema wafanyakazi wa kiwanda hicho ambacho zamani kilikuwa kinaitwa Southern Paper Mills (SPM), waliamua kufungua kesi mahakamani wakashinda na iliamriwa walipwe fidia lakini Serikali ikakata tena rufaa. “Nikiwa mbunge niliamua kuzungumza na Serikali, ikakubali kuwalipa kama alivyoahidi mgombea leo hapa,” alisema Kigola anayetetea kiti hicho kwa awamu ya pili.
Mkazi wa eneo hilo, John Kibiki alisema endapo Serikali itatekeleza ahadi hiyo, itakuwa imewasaidia kutua mzigo mkubwa.
Naye Neema Tanda aliunga mkono kauli hiyo na kusema wanasubiri utekelezaji.






SOURCE:Mwananchi





























Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

USAJILI WENYE MANUFAA EPL HADI SASA..