CCM Mwanza, Ukawa Dar...
Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli akiagana na mtoto wakati akiondoka katika Uwanja wa Bwawani, baada ya kuwahutubia wakazi wa Kibaha mkoani Pwani jana.
Katika kuhakikisha wanaitumia siku hiyo vyema, wagombea wanaochuana vikali, Edward Lowassa wa Chadema na Dk John Magufuli wa CCM wamekuja na staili tofauti inayoashiria saa za majeruhi.
Wakati Lowassa akimaliza kampeni kwenye viwanja vya Jangwani kuanzia saa 6:00 mchana hadi saa 9:00 alasiri, Dk Magufuli atahitimisha kampeni zake mkoani Mwanza, huku vigogo wa chama hicho, wakiongozwa na marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa wakifanya mikutano katika mikoa saba tofauti siku hiyo.
CCM pia imebainisha kuwa siku ya uchaguzi itakuwa na matokeo yote ya uchaguzi huo itakapofika saa nne usiku baada ya kuyakusanya kupitia mawakala wake katika vituo vyote nchini.
Lowassa Dar
Akizungumza jijini jana, kaimu katibu mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu alisema Lowassa atahitimisha kampeni hizo mapema, ili apate nafasi ya kwenda nyumbani kwake Monduli mkoani Arusha kupigakura Jumapili.
“Tunaomba wanachama, mashabiki, wapenzi na wafuasi wa Chadema na vyama vinavyounda Ukawa kujitokeza mapema kwenye viwanja vya Jangwani,” alisema Makene.
“Wanatakiwa kufika pale kuanzia saa 3:00 asubuhi na tutaanza mkutano saa 6:00 mchana. Tunataka kumaliza mapema ili Lowassa awahi kuondoka na wananchi pia warudi mapema majumbani mwao kujiandaa kupigakura Jumapili,” alisema Mwalimu.
Mikutano mingi ya kufunga kampeni imekuwa ikifanyika jioni lakini Mwalimu alisema limefanyika mahsusi kwa ajili ya kutoa nafasi kwa mgombea wao wa urais na wananchi.
Alisema viongozi wakuu wa Ukawa watakuwapo katika mkutano huo, huku akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi Jumapili kumpigia kura Lowassa ili kutimiza ndoto ya mabadiliko.
Lowassa kuhutubia Taifa leo
Wakati huohuo, leo Lowassa atahutubia Taifa kupitia vituo mbalimbali vya televisheni, redio na njia nyingine za upashanaji habari, hususan mitandao ya kijamii kuanzia saa 3:00 usiku.
Taarifa ya mkuu wa Idara ya Habari Chadema, Tumaini Makene inasema katika hotuba hiyo, Lowassa atazungumza kuhusu Tanzania mpya itakayotokana na mabadiliko makubwa ya kimfumo, kiutawala na utendaji wa serikali endapo atapata dhamana ya kuwa mkuu wa nchi, amiri jeshi mkuu na kiongozi mkuu wa Serikali.
Lowassa aahidi ushindi
Akiwa Handeni na Kilindi, Waziri huyo mkuu wa zamani, alisema ametembea mikoa mbalimbali na kwa tathmini yake ushindi utapatikana.
Katika mkutano wa Handeni, Lowassa ambaye aliwataka wakazi kusimama kwa dakika moja kumkumbuka mbunge wa jimbo hilo, Dk Abdallah Kigoda aliyefariki nchini India alikokuwa akitibiwa, alisema atakuwa rais wa vitendo na si wa maneno.
“Nitapata ushindi wa asilimia 80 na nikiingia madarakani, nitaleta mabadiliko katika maisha,” alisema.
Alisema mabadiliko atakayofanya ni pamoja na elimu bure kuanzia chekechea hadi chuo kikuu kwa kuwa rasilimali za kufanya hivyo, zipo ikiwemo misamaha ya kodi.
Fomu ya matokeo
Wakati huohuo, Chadema na Ukawa wamesema wamenasa fomu ya matokeo ya uchaguzi wa rais iliyoongezwa kipengele cha “idadi ya wapigakura walioongezeka” na hivyo kutofautiana na mfano wa fomu halisi uliopo katika kanuni za uchaguzi mwaka 2015 zilizosainiwa na vyama vyote vya siasa.
Kutokana na kuibaini suala hilo, umoja huo umeitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutoa ufafanuzi wa kina, kusisitiza kuwa Ukawa utazitambua fomu zinazofanana na zile za mfano zilizopo katika kanuni hizo.
Hata hivyo, mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva aliliambia gazeti hili kuwa Chadema wanapaswa kuwasilisha malalamiko yao kwa maandishi, hivyo hawezi kusema iwapo kilichopo katika fomu hiyo ni kweli au si kweli kwa maelezo kuwa wakati anazungumza na mwandishi wetu hakuwa na mfano wa fomu hiyo.
Dk Magufuli Mwanza
Kwa upande wake, Dk Magufuli atakuwa mkoani Mwanza, kwa mujibu wa mjumbe wa kamati ya kampeni za CCM, January Makamba ambaye alisema mkutano huo utarushwa moja kwa moja na vyombo mbalimbali vya habari.
Alisema katika mkutano wa Dk Magufuli ambaye atakuwa na mgombea mwenza, Samia Suluhu na Rais Jakaya Kikwete, zitafungwa runinga kubwa zitakazoonyesha matukio ya mikutano mingine saba ya chama hicho itakayokuwa ikifanyika katika mikoa mingine.
“Mikutano hii yote itaanza saa 6:00 mchana na itarushwa yote kwa pamoja kwa matangazo ya moja kwa moja kupitia televisheni tano na redio 67 nchini,” alisema.
Alisema mkutano mingine itafanyika mkoa wa Tanga, ukiongozwa na katibu mkuu wa CCM, Abrahamani Kinana, huku Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa akiongoza mkutano utakaofanyika Mbeya.
Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi ataongoza mkutano wa Mtwara, huku Makamu mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula akiongoza mkutano utakaofanyika Kigoma.
Mkoani Kilimanjaro, Katibu mkuu mstaafu wa chama hicho, Yusuf Makamba ataongoza mkutano huku mwenyekiti wa Iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba akiongoza mkutano utakaofanyika mkoani Mara.
Makamba alisema kuwa namna hii ya ufungaji wa kampeni inadhihirisha nguvu ya CCM inayoiwezesha kufanya mikutano mikubwa mingi kwa siku moja katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa upande wa Dar es Salaam, chama hicho leo kitafanya mkutano kwenye viwanja vya Jangwani na kesho wagombea wake wa ubunge mkoani humo watafunga kampeni kwa kufanya mikutano mikubwa katika majimbo yao.
Pamoja na taarifa hiyo ya mikutano ya kufungia kampeni, chama hicho kimetoa tathmini yake kwa kampeni za mwaka huu na kudai kuwa kimeridhika na ubora na ukubwa wa kampeni zake.
“Dk Magufuli na Samia Suluhu wamefanya kazi kwa bidii na maarifa makubwa. Wamekuwa barabarani kwa siku 57, wakifanya mikutano kati ya nane hadi 12 kwa siku. Imani yetu ya ushindi inatokana na kazi yao kubwa,” alisema Makamba.
Chama hicho pia kimeendelea kusisitiza uchaguzi wa amani na utulivu, kikisisitiza vyama vingine kufanya hivyo.
“Sisi kama chama kikubwa cha siasa nchini chenye wafuasi wengi zaidi na chenye dhamana ya uongozi wa dola, tutatimiza wajibu wetu kuhimiza utulivu kwa wapenzi, washabiki na wanachama wetu.
“Kauli za wenzetu kwamba kura zitaibiwa ni kauli za kutojiamini na kujiandaa kufanya vurugu na si kauli za wanaotaka uchaguzi wa amani.”
Aidha mjumbe huyo wa kamati ya kampeni alisema Jumamosi chama chake kitatangaza namba maalum za simu kwa Watanzania wote ili waweze kupiga simu au kutuma ujumbe pale watakapobaini vitendo au viashiria vya kuvuruga amani siku ya uchaguzi na mara baada ya uchaguzi.
Magufuli kulinda rasilimali
Akizungumza kwenye kampeni, Dk Magufuli alisema sababu ya kuamua kugombea urais ni kutaka kuzilinda rasilimali za Watanzania.
Akizungumza jana na wananchi wa Kibaha, Pwani na baadaye, kata ya Bunju, Dar es Salaam, Dk Magufuli alisema yeye hafanyi siasa bali malengo yake ni kufanya kazi na kuinua uchumi wa Taifa.
Alisema katika miaka 20 ya uwaziri amejifunza na kuyajua matatizo na changamoto za Watanzania na kuwa wananchi wampe kura awafanyie kazi.
“Mimi sifanyi siasa, na nakiri mimi si mwanasiasa mzuri ndio maana unaona naweza kusema CCM imejaa mifisadi na wengine wameanza kunikimbia. Nawahakikishia mimi nikiwa Rais nitafanya kazi ya kusimamia rasilimali zenu na wananchi watanufaika nazo,” alisema Magufuli.
Alisema kati ya mambo yanayomkera ni wananchi maskini kunyanyaswa kwa kutozwa kodi katika kila biashara wanazofanya huku matajiri na wafanyabiashara wakubwa wakineemeka na kukwepa ushuru.
“Nataka Watanzania maskini wapumue na waifurahie nchi yao. Nichagueni niwe rais, nitahakikisha naondoa ushuru kwa wafanyabiashara wadogo, nitaondoa ushuru kwenye saluni, maduka, wauzaji wa mbogamboga, wenye maduka wote hawa ni watu maskini wanaofanya biashara ili kujikomboa katika maisha ya umasikini,” alisema Magufuli.
Imeandikwa na Maimuna Kubegeya, Fidelis Butahe, Joyce Mmasi, Juliet Ngarabali, Ibrahim Bakari na Rajab Athumani
Maoni
Chapisha Maoni